Yanga yazindua rasmi ujenzi wa jengo lao

DAR ES SALAAM: KLABU ya Yanga imetangaza rasmi kuanza mchakato wa ujenzi wa jengo jipya la Yanga Tower, Mtaa wa Mafia na Nyamwezi, Kariakoo.
Yanga imeeleza hayo leo Jumatano kwenye hafla fupi ya uingiaji mkataba wa mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 5.5.
Imefafanuliwa kuwa Benki ya Azania ndiyo mfadhili mkuu na muwezeshaji wa kifedha katika ujenzi huo ambao umekabidhiwa kwa Kampuni ya Group Six International walioshinda zabuni ya ukandarasi wa mradi huo.
Rais wa Yanga, Mhandisi Hersi Said alisema jengo hilo litakuwa na ghorofa 12 na linatarajia kukamilika ndani ya miezi 12 kwa kuzingatia ubora na thamani ya fedha iliyowekwa.

“Jengo hili limeundwa kwa kuzingatia mahitaji ya Kariakoo pamoja na mahitaji ya taasisi yetu.
“Basement itatumika kwa ajili ya maduka na shughuli nyingine za kibiashara. ‘Ground floor’ na ghorofa ya kwanza itakuwa na maeneo ya biashara, hususan maduka.
“Kuanzia ghorofa ya pili hadi ya kumi ni kwa ajili ya maghala ya kuhifadhi bidhaa. Ghorofa ya 11 na 12 zitatumika kwa ajili ya makazi.
“Na katika ghorofa ya 13 ambayo ndiyo ‘rooftop’, tumepanga kuweka eneo maalum kwa ajili ya sehemu ya kupumzika, kupata kahawa na chakula, kutazama michezo kufanya mikutano na kukutana na watu mbalimbali,” alifafanua Said.




