Ligi Kuu

Ibenge awaita mashabiki kuiunga mkono Azam FC

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge, amewataka mashabiki wa timu hiyo kuendelea kujitokeza kwa wingi uwanjani kuiunga mkono katika kila mchezo, akisisitiza kuwa kikosi chake kinalenga kushinda kila kinaposhuka dimbani.

Ibenge alitoa kauli hiyo jana baada ya Azam FC kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Namungo katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Ibenge amesema ushindi ni lengo la kila mchezo, lakini timu inapaswa kuwa tayari kujipanga upya endapo matokeo hayatakuwa mazuri huku akizungumzia umuhimu wa mashabiki kujitokeza kuwapa nguvu wachezaji.

“Michezo yote tunataka kushinda, lakini ikitokea hatujashinda, hakuna tatizo. Tutarudi kujipanga tena na kufanya kazi kwa bidii. Huu ni wakati wa mashabiki wetu kuja kutusapoti ili tushinde na kufurahi pamoja” amesema.

Amesema kabla ya kila mchezo, wachezaji wake hupewa msisitizo wa kupambana kutafuta ushindi, huku akitambua kuwa kila timu huingia uwanjani ikiwa na mbinu zake.

Ibenge alitolea mfano Namungo, akisema wapinzani wao walitumia mbinu ya kujilinda na kufanya mashambulizi ya kushtukiza, jambo alilolieleza kuwa ni hatari kwa timu pinzani.

Kocha huyo pia alitumia nafasi hiyo kuwaalika mashabiki wa Azam FC kuendelea kujitokeza uwanjani ili kuipa timu hiyo hamasa katika michezo yake ijayo.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button