EPL

Barker: Hatujamaliza Kazi

DAR ES SALAAM: USHINDI wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Mighty Wanderers ya Malawi umeipa Simba SC matumaini ya kutinga hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini Kocha Mkuu Steve Barker amesema bado hawajamaliza kazi, akiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi katika mchezo wa marudiano Jumapili.

Barker alitoa kauli hiyo jana baada ya kikosi cha Simba kurejea nchini kikitokea Malawi, huku akisisitiza kuwa ushindi wa ugenini haupaswi kuwafanya waridhike kabla ya mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

“Pamoja na kwamba tumeshinda ugenini bao 1-0, hatupaswi kuridhika. Tunahitaji kumaliza kazi salama na kuvuka hatua inayofuata,” amesema Barker.

Kocha huyo amesema kikosi chake kinahitaji kuhakikisha kinapata matokeo yatakayoiwezesha kuendelea na safari ya mashindano hayo, akiwataka mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Uhuru ili kuwapa wachezaji hamasa katika kuwania ushindi.

Barker amesema pamoja na ushindi huo, bado kuna mapungufu katika kiwango cha timu ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi ili yasijirudie katika mchezo wa marudiano dhidi ya Mighty Wanderers.

“Mimi kama kocha siwezi kuridhishwa kwa asilimia 100 na kiwango. Lazima kuna mapungufu ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi ili yasijirudie katika mchezo wa marudiano,” amesema.

Wakati huo huo, Barker amethibitisha kuwa winga mshambuliaji Libasse Gueye atakuwa sehemu ya kikosi kitakachocheza mchezo huo wa marudiano.

Related Articles

Back to top button