A-List wakiri makosa, waahidi kurekebisha maudhui

DAR ES SALAAM: WASANII wa filamu nchini, Irene Uwoya, Jacqueline Wolper, Frida Masanja ‘Kajala’ na Aunty Ezekiel, ‘A-List’, wameahidi kufanya maboresho ya maudhui katika kipindi chao baada ya kuelimishwa na Bodi ya Filamu Tanzania kuhusu umuhimu wa kuzingatia maadili ya Kitanzania.
Wasanii hao wametoa kauli hiyo baada ya kuitikia wito wa Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga, aliyekutana nao na kujadili baadhi ya masuala ya kimaadili yaliyojitokeza katika kipindi chao kinachorushwa kupitia televisheni na mitandao ya kijamii.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Irene Uwoya amesema moja ya mambo waliyosisitiziwa ni umuhimu wa kutumia tafsida katika baadhi ya maudhui yao ili kupunguza makali ya lugha na kuhakikisha maudhui yanayowasilishwa yanazingatia maadili, mila na desturi za Kitanzania.
“Uzuri ni kwamba wameongea nasi kama watoto wao. Hawakuongea kwa ukali, bali wametuelimisha pale ambapo tumekosea. Tumeelewa makosa yetu na tuko tayari kuyarekebisha,” amesema Uwoya.
Amesema wamefurahishwa na namna Bodi ya Filamu ilivyowapokea na kuwapa maelekezo, akibainisha kuwa mazungumzo hayo yalilenga kuwasaidia kuboresha kazi yao.
“Kwa zaidi, wanapenda A-List na wanapenda kipindi chetu. Wameona ni kipindi kizuri sana, hivyo wametuelekeza maeneo ambayo tunatakiwa kuyarekebisha na jambo hilo tumelifurahia sana,” amesema.
Uwoya ameongeza kuwa wao wanaichukulia Bodi ya Filamu kama mlezi mwenye jukumu la kuwaongoza na kuwasahihisha pale wanapokosea.
“Wao ni walezi wetu, wametuelekeza na tumepokea maelekezo yao. Tunakiri makosa yetu na tuko tayari kujirekebisha,” amesema.
Kauli hiyo imekuja baada ya Bodi ya Filamu Tanzania kuwataka waigizaji hao kufanya marekebisho katika baadhi ya maudhui ya kipindi cha A-List, ili kuhakikisha yanaakisi na kuheshimu maadili, utamaduni, mila na desturi za Kitanzania.




