Kasongo avionya vilabu ligi kuu, ataka visilaumu baadaye
DAR ES SALAAM: MTENDAJI Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB), Almas Kasongo, amezitaka klabu kufanya marekebisho ya viwanja kipindi hiki cha ‘pre season’ ili kuepuka kufungiwa katikati ya ligi itakapoanza.
Mtendaji huo ameliambia Spotileo, kuwa kabla ya ligi kuanza viwanja vyote vitakaguliwa na hakuna uwanja ambao utaruhusiwa kutumika kama utakuwa haujakidhi matakwa ya kanuni.
Baadhi ya viwanja vilivyofungiwa msimu uliopita kutokana na ‘pitch’ yake kutokuwa na viwango vya kuchezea ni Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, na Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni Dar es Salaam.
“Miongoni mwa ajenda kubwa ni miundombinu, ligi yetu inatakiwa ichezwe katika viwanja bora, makusudio ni msimu ujao unatakiwa viwanja vyote viwe bora hivyo klabu zinapaswa kufanya marekebisho ili kuweza kukidhi matakwa ya kikanuni,” amesema Kasongo.
Mtendaji huyo amesema timu zinazomiliki viwanja zinatakiwa kuhakikisha zinaimarisha kuwa bora na kukidhi vigezo ili mchezaji aweze kuwa huru anapokuwa uwanjani.
Amesema klabu zinatakiwa kupambana kuhakikisha wanakuwa na viwanja bora kuepuka usumbufu wa kukiuka kanuni na sheria 17 za mpira wa soka.
“Muhimu kufanyia marekebisho eneo la kuchezea vinapokuwa vibovu vinasababisha ligi kupunguza mvuto na kushusha hadhi, tumekuwa tukipambana kila klabu yenye kiwanja kuwakumbusha kufanya marekebisho,” amesema Kasongo.