Mastaa

Steve Nyerere: Msimuache Rais Samia peke ake

DAR ES SALAAM: WASANII nchini wametakiwa kuungana kwenda Zanzibar kumfariji na kutoa pole kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kufuatia msiba wa mume wake, Hafidhi Ameir Hassan.

Mwito huo umetolewa Leo na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao Steven Mengele ‘Steve Nyerere’ huku akieleza kuwa msiba wa mtu muhimu katika familia unahitaji faraja kutoka kwa ndugu, marafiki na watu mbalimbali waliokuwa karibu na familia hiyo.

Akizungumza kuhusu msiba huo, Steve Nyerere’ amesema Dk. Samia amepoteza mtu ambaye hakuwa tu mume wake, bali pia alikuwa baba, mshauri na mtu muhimu katika maisha yake pamoja na familia.

“Tumepoteza mtu muhimu. Alikuwa baba, alikuwa mshauri na mwongoza maono katika familia na hata katika jamii. Kwa hiyo, tunatoa pole kwa familia, Watanzania na ndugu zetu wa Zanzibar,” amesema.

Amesema si vyema wasanii na makundi mbalimbali kujitokeza kwa wingi wakati wa kampeni, ziara za viongozi, uzinduzi wa miradi au shughuli za burudani pekee, bali wanapaswa pia kuwa karibu na viongozi na watu waliowasaidia katika nyakati za majonzi.

Aidha, amewataka wasanii wa Bongo Fleva na wasanii wengine kutumia nafasi hiyo kwenda Zanzibar kushiriki katika kutoa pole, akieleza kuwa safari hiyo inaweza kufanyika hata kwa muda mfupi.

“Zanzibar si mbali. Unaweza kwenda asubuhi na kurudi. Ni jambo la kawaida kwenda kumfariji mtu aliyepatwa na msiba. Tumefundishwa katika dini zetu kwamba kumstiri na kumfariji mtu aliyefiwa ni ibada,” amesema.

Amesema wasanii wanapaswa kujenga utamaduni wa kuwa karibu na watu wanaowafungulia milango na kuwasaidia katika shughuli zao, akisisitiza kuwa maisha yana mzunguko na wakati mwingine mtu anayemsaidia mwingine leo anaweza kuhitaji msaada na faraja kesho.

Related Articles

Back to top button