Nyumbani

Prisons ya moto yaanza kusukwa

MBEYA: UONGOZI wa klabu ya Tanzania Prisons yenye maskani yake mkoani Mbeya umeweka wazi tetesi za kuketi mezani na kocha Mbwana Makata kuinoa timu hiyo akichukuwa nafasi ya Ahmad Ally ambaye walitangaza kuachana naye.

Baada ya kuachana na Ahmed Ally wajelajela hao sasa wameanzisha mazungumzo na kocha Makata ambaye hivi karibuni ameisaidia timu Pamba Jiji FC, kurejea Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024/2025

Akizungumza na Spotileo, Katibu Mkuu wa Tanzania Prisons, Ajabu Kifukwe amesema baada ya makubaliano ya pande zote mbili kuachana na kocha waliyekuwa naye msimu uliopita wakati wowote wanatarajia kumtambulisha Makata.

Amesema Makata atakuwa sehemu benchi la ufundi la timu hiyo na atashirikiana na viongozi kwenye masuala yote ya usajili wa wachezaji wapya.

“Tumeshamalizana na Makata na Msaidizi wake kesho (Jumatatu) tutaanza rasmi kufanya usajili wachezaji wapya kulingana na mapendekezo ya benchi la ufundi pamoja na mapungufu ya kikosi chetu,” amesema Kifukwe.

Akizungumzia kikosi Kifukwe amesema hakutakuwa na mabadiliko makubwa katika kikosi na watafanya usajili kulingana na mahitaji yao ambayo ni kipa, beki na mshambuliaji maeneo ambayo wanaona yana mapungufu.

Katibu huyo amesema safari hii wataangalia zaidi wachezaji wazawa kuimarisha timu yao kufanya vizuri msimu ujao wa Ligi hiyo.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button