Tanzanite Queens kuivaa England leo

BIELSKO BIALA: BAADA ya kuanza kwa kichapo cha mabao 4-1 dhidi ya Brazil, Tanzanite Queens inarudi uwanjani leo ikiwa na kazi ya kusaka matokeo yatakayoipa matumaini ya kuendelea na safari yake ya kihistoria katika Kombe la Dunia la Wanawake U-20 dhidi ya England.
Mchezo huo wa Kundi B utakaochezwa Uwanja wa Miejski, Bielsko-Biała nchini Poland, ni muhimu kwa Tanzania, ambayo inashiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza. England nayo iliingia kwenye mashindano hayo kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Canada, hivyo kila timu inatafuta ushindi wake wa kwanza.
Tanzanite Queens ilianza vizuri dhidi ya Brazil kwa kusawazisha bao kupitia penalti ya Winfrida Gerald, lakini wapinzani hao waliongeza kasi kipindi cha pili na kufunga mabao matatu zaidi.

Kocha Bakari Shime amesema mchezo huo umekuwa somo kwa timu yake, huku akisisitiza kuwa amefanyia kazi mapungufu anaamini watafanya vizuri.
Kwa upande wa England, sare dhidi ya Canada imeifanya timu hiyo kuingia kwenye mchezo huu ikihitaji ushindi ili kuongeza nafasi ya kufuzu hatua ya 16 bora.
Tanzania nayo inahitaji kuboresha kiwango chake, hasa katika kudhibiti mashambulizi ya wapinzani na kutumia vizuri nafasi zitakazopatikana.
Mchezo huu unatarajiwa kuwa mtihani mwingine kwa vijana hao wa Tanzania, lakini pia ni nafasi ya kuonesha kuwa kufuzu kwao Kombe la Dunia hakukuwa kwa bahati. Baada ya England, Tanzanite Queens itamaliza hatua ya makundi dhidi ya Canada Septemba 11.




