Ligi Kuu

Mngqithi: Tutafuzu hatua inayofuata

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi, amesema kikosi chake kipo tayari kupambana kwa nguvu katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ya Botswana, akisisitiza kuwa ushindi ndio unaowapa nafasi ya kutinga hatua inayofuata.

Yanga ilitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Botswana, hivyo inahitaji ushindi au sare ya 0-0 katika mchezo wa marudiano ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele.

Akizungumza kuelekea mchezo huo, Mngqithi amesema timu yake itaendelea kutumia mbinu ilizozoea, huku ikilenga kuwalazimisha wapinzani kufanya makosa na kuyatumia kupata mabao.

“Tutafanya yale tuliyozoea kufanya, tutawalazimisha wapinzani wetu kufanya makosa na kuwaadhibu. Hakuna kilichobaki zaidi ya sisi kushambulia kwa wingi na kuamini mchakato,” amesema Mngqithi.

Kocha huyo amesema anaamini timu yake inaendelea kuimarika kila siku na kwamba wachezaji wake wana uwezo wa kufanya vizuri katika mchezo huo muhimu.

“Naamini timu inaimarika kila siku na naamini tutafuzu hatua nyingine,” amesema.

Katika hatua nyingine, Meneja Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, ametangaza viingilio vya mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam.

Kamwe amesema mashabiki wataingia kwa Sh 5,000 kwa viti vya mzunguko, Sh 10,000 na kiwango cha juu cha Sh 30,000.

Pia, amesema mchezo huo utakuwa ni siku maalum ya kumkaribisha Seleman Mwalimu Jangwani kwa kuwa alifanya jambo la maana kule Botswana kwa kuisawazishia timu hiyo ilipokuwa nyuma bao 1-0.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa wa ushindani mkubwa kutokana na umuhimu wake kwa timu zote mbili, huku Yanga ikihitaji kutumia vizuri nafasi ya kucheza nyumbani ili kutimiza lengo la kutinga hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Related Articles

Back to top button