Aziz Ki amkataa Mobetto
KIUNGO wa Yanga, Stephane Aziz Ki ameweka wazi kwa wale wanaocheka juu ya kuacha ofa kubwa ya klabu ya CR Belouizdad ya Algeria na kusalia Yanga kwa ajili ya mapenzi na msanii Hamisa Mobetto.
Amesema amebakia yang kwa ajili ya mapenzi na timu hiyo na sio kwa ajili ya mwanamke, kwa kuwa alikuja nchini na mama yake na kusaini mkataba wa kusalia kucheza timu hiyo baada ya makubaliano ambayo amewekeana na Rais wa Yanga, Hersi Said.
Ilidaiwa kuwa Aziz Ki alikataa ofa ya klabu ya CR Belouizdad ambayo iliweka wazi ipo tayari kumpa mshahara mkubwa na baadhi ya vitu ikiwemo nyumba na tiketi ya ndege ya daraja la juu.
Kiungo huyo amesema hakuna mtu aliyemlazimisha kubaki Yanga bali ni mapenzi yake na kuhakikisha yale waliyoahidiana na Hersi yanafikwa ikiwemo kucheza fainali ya Afrika.
“Niko hapa Yanga kwa ajili ya mapenzi yangu na timu na sio kwa ajili ya Hamisa Mobetto . Najisikia furaha kucheza hapa, kukutana na Clatous Chama na Prince Dube, wamekuwa na msimu bora hapo nyuma.
Kuhusu safari ya Afrika Kusini, kiungo huyo amesema wanaenda kucheza na timu kubwa na kila mmoja ana ndoto ya kucheza na timu hizo, anaamini yatakuwa maandalizi mazuri kwao kwa ajili ya msimu wa 2024/25 wa mashindano.
Yanga tayari imewasili nchini Afrika Kusini ambapo walipata mwaliko wa kucheza mashindano ya Mpumalanga na watacheza dhidi ya FC Augsburg inayoshiriki Bundesliga, Julai 20 na 24 mwaka huu na kisha itacheza na TS Galaxy FC.