Bodi ya Filamu yawaonya waigizaji kuzingatia maadili

DAR ES SALAAM: BODI ya Filamu Tanzania imewataka waigizaji nchini kuzingatia maadili, mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania katika kazi zao, hususani wanapozalisha maudhui yanayowafikia wananchi kupitia televisheni na mitandao ya kijamii.
Wito huo umetolewa na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga, alipokutana na waigizaji Aunty Ezekiel, Irene Uwoya, Jacqueline Wolper na Frida Kajala, kufuatia wito uliotolewa kwa wasanii hao kufika katika ofisi za bodi jana, Jumatatu, Septemba 7, 2026.
Katika kikao hicho, Dkt. Kasiga alieleza masuala ya kimaadili yaliyojitokeza katika kipindi cha “A-List”, kinachorushwa kupitia televisheni na mitandao ya kijamii.
Amewataka waigizaji hao kufanya marekebisho yanayostahili katika maudhui ya kipindi hicho ili kuhakikisha yanaakisi na kuheshimu maadili, mila, desturi pamoja na utamaduni wa Kitanzania.
Aidha, Dkt. Kasiga amewakabidhi waigizaji hao kitabu cha mkakati wa taifa wa kukabiliana na mmomonyoko wa maadili wa miaka 10, kilichotolewa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Amesema kitabu hicho kinapaswa kuwa rejea muhimu kwa wasanii na watayarishaji wa maudhui katika uandaaji na uzalishaji wa kazi zinazowasilishwa kwa umma kupitia filamu, vipindi vya televisheni na majukwaa mengine.
Kwa upande wao, waigizaji hao walikiri kuwepo kwa baadhi ya makosa ya kimaadili katika kipindi hicho, wakaomba radhi na kuahidi kufanya maboresho yanayostahili.

Wamesema watahakikisha maudhui yatakayowasilishwa katika kipindi hicho yanaendana na maadili, utamaduni, mila na desturi za Kitanzania.
Dkt. Kasiga amewakumbusha waigizaji hao umuhimu wa kuzingatia maadili katika utekelezaji wa kazi zao, akisisitiza kuwa wasanii wana nafasi kubwa katika jamii kutokana na ushawishi wa kazi wanazozalisha kwa wananchi.
Pia amebainisha kuwa mamlaka nyingine za Serikali zinazohusika na usimamizi wa vipindi vya televisheni zinaendelea kufuatilia maudhui yanayorushwa, huku akiwataka wadau wote wa sekta ya filamu na burudani kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na maadili ya nchi.




