Katambi atoa onyo kwa wasanii

DAR ES SALAAM: Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi, amewafutia makosa wasanii na watengeneza maudhui mtandaoni waliokuwa wakikabiliwa na makosa mbalimbali yanayodaiwa kuhusiana na ukiukwaji wa taratibu na maadili nchini.
Akizungumza jana, Katambi amesema wasanii na watengeneza maudhui hao wamepewa nafasi nyingine baada ya makosa yao kufutwa, huku wakipewa semina ya maadili ili kuwasaidia kuelewa wajibu wao kwa jamii na Taifa.
Amesema hatua hiyo imechukuliwa kwa lengo la kutoa nafasi kwa wasanii na watengeneza maudhui kujirekebisha na kutumia vipaji na majukwaa yao kwa njia yenye manufaa kwa jamii.
Katambi amewataka watengeneza maudhui kutotengeneza maudhui kwa lengo la kupata “views” na malipo pekee bila kuzingatia madhara yanayoweza kusababishwa na maudhui hayo kwa jamii.
“Usiweke kontenti ili tupate view ili ulipwe bila kujali kuwa unaleta athari kwenye jamii na Taifa kwa ujumla,” amesema Katambi.
Aidha, Waziri huyo ametoa onyo kwamba baada ya wito huo, msanii au mtengeneza maudhui yeyote atakayekiuka sheria atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria husika.
“Baada ya wito huu, yeyote atakayevunja sheria atachukuliwa hatua za kisheria kama hawezi kujenga maadili ya Taifa letu,” amesema.
Katambi pia amewataka wananchi na wadau wa sanaa kutumia njia sahihi pale wanapoona msanii amekosea, badala ya kuchukua hatua wenyewe.
“Msanii anapokosea, mpeleke sehemu husika na atahudumiwa kulingana na sheria husika,” amesema.





One Comment