Shemndolwa, Ondari mabingwa mashindao ya gofu ya Vodacom 2026

DAR ES SALAAM: Khalid Shemndolwa na Yvonne Ondari wameibuka mabingwa wa jumla katika mashindano ya gofu ya Vodacom Corporate Masters 2026 yaliyofanyika katika Uwanja wa TPDF Lugalo Golf Club jijini Dar es Salaam.
Shemndolwa alitwaa ubingwa kwa upande wa wanaume baada ya kukusanya pointi 42 katika mashindano hayo ya siku moja, huku Ondari akifikisha idadi hiyo hiyo ya pointi na kutwaa ubingwa kwa upande wa wanawake.
Mashindano hayo yaliwakutanisha takribani wachezaji 150 kutoka Tanzania na nchi jirani, huku ushindani ukiwa mkali katika madaraja mbalimbali.

Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando (kushoto), akikabidhi zawadi ya tiketi ya kwenda na kurudi Mauritius kwa mshindi wa jumla kwa wanaume Khalid Shemndolwa (wa tatu kushoto) katika mashindano ya Vodacom Corporate Masters 2026 Golf Tournament yaliyofanyika Lugalo Golf Club, Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki.
Katika daraja A, Godfrey Abel alimaliza kinara baada ya kupata pointi 42, akifuatiwa na Likuli Juma aliyefikisha pointi 41.
Sigfrid Urassa alitwaa ubingwa wa daraja B kwa pointi 40, akimzidi Godfrey Kilenga aliyepata pointi kama hizo. Urassa alipewa ushindi kwa kutumia kanuni ya countback.
Kwa upande wa daraja C, Boniface Japhet alitwaa ubingwa baada ya kukusanya pointi 39, huku Abdallah Singano akimaliza nafasi ya pili kwa pointi 37.
Kwa wanawake, Neema Job alimaliza katika nafasi ya kwanza akiwa na pointi 42, huku Leticia Kapalia akishika nafasi ya pili baada ya kupata pointi 40.

Mshindi wa jumla kwa upande wa wanawake, Yvonne Ondari (wa tatu kushoto), akipokea zawadi baada ya kutwaa taji katika Vodacom Corporate Masters 2026 Golf Tournament yaliyofanyika Lugalo Golf Club mwishoni mwa wiki. Ondari alikusanya pointi 42 (CB) katika mashindano yaliyoshirikisha wachezaji golf 150 kutoka Tanzania na nje ya nchi.
Katika tuzo za uchezaji binafsi, Michael Norbert alitwaa tuzo ya Longest Drive kwa wanaume, wakati Kapalia alishinda tuzo hiyo kwa wanawake. Harshid Barmeda alitwaa Nearest to the Pin kwa wanaume, huku Vaileth James akishinda kwa wanawake.
Katika mashindano ya timu za kampuni, timu ya KQ iliibuka mshindi baada ya kushindana dhidi ya timu nyingine tisa.
Mbali na ushindani wa uwanjani, mashindano hayo yaliambatana na shughuli mbalimbali katika eneo la Corporate Village, ambako washiriki na familia zao walipata fursa ya kushuhudia burudani, maonesho ya biashara, magari ya zamani pamoja na eneo maalum la watoto.

Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando, akishiriki mashindano ya Vodacom Corporate Masters 2026 Golf Cup yaliyofanyika Lugalo Golf Club, Dar es Salaam, Septemba 5, 2026. Mashindano hayo yalishirikisha wachezaji gofu 150 kutoka Tanzania na nje ya nchi.
Mkurugenzi wa Vodacom Business wa Vodacom Tanzania PLC, Nguvu Kamando, alisema mashindano hayo yameendelea kuonyesha umuhimu wa michezo katika kuwakutanisha watu na kujenga mahusiano.
“Vodacom Corporate Masters 2026 Golf Cup imethibitisha tena kwamba michezo ni jukwaa lenye nguvu katika kujenga mahusiano ya muda mrefu ya kibiashara. Tunafurahishwa na ushiriki mkubwa wa kampuni na kasi ya mahusiano mapya yaliyojengwa wiki hii,” alisema Kamando.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Corporate Masters, Ken Kariuki, alisema ushindani wa mwaka huu ulikuwa wa kiwango cha juu na kwamba mashindano hayo yanaendelea kutoa jukwaa kwa wachezaji kukutana na kuendeleza mchezo wa gofu.

Mkuu wa Idara ya Masoko na Uwezeshaji wa Vodacom Business Joseph Sayi, akishiriki mashindano ya Vodacom Corporate Masters 2026 Golf Cup yaliyofanyika Lugalo Golf Club, Dar es Salaam, Septemba 5, 2026. Mashindano hayo yalishirikisha wachezaji gofu 150 kutoka Tanzania na nje ya nchi.
“Mwaka huu tulishuhudia ushindani wa kiwango cha juu uwanjani na ushiriki wenye maana katika biashara nje ya uwanja.
Hilo ndilo lengo kuu la Corporate Masters, kuzikutanisha kampuni katika mazingira rafiki yanayozalisha fursa halisi za ushirikiano,” alisema Kariuki.
Alisema ushirikiano kati ya Vodacom na Corporate Masters unaonyesha namna kampuni zinavyoweza kufanya kazi pamoja katika kutengeneza thamani kwa wateja na wadau, huku zikiunga mkono maendeleo ya mchezo wa gofu nchini Tanzania.
Kwa ushindi wa Shemndolwa na Ondari, pamoja na matokeo ya kuvutia katika madaraja mbalimbali, Vodacom Corporate Masters 2026 imehitimishwa kwa ushindani mkubwa katika uwanja wa Lugalo, huku mchezo wa gofu ukiendelea kupata jukwaa la kuwakutanisha wachezaji kutoka Tanzania na nchi jirani.




