Nyumbani

Nsangazelu aipa tano TFF kwa Mfumo wa kuzalisha vipaji

DAR ES SALAAM:KOCHA Mkuu wa Serengeti Boys, Elieneza Nsangazelu, amesema mafanikio yaliyopatikana na timu hiyo katika michuano ya AFCON ya vijana ni matokeo ya maandalizi mazuri pamoja na uwekezaji uliofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika kukuza vipaji vya vijana.

Nsangazelu amesema awali watu wengi hawakuwa na imani kuwa Tanzania ingeweza kufanya vizuri katika mashindano hayo, lakini maandalizi ya muda mrefu na uwepo wa vituo vya kukuza vipaji umeonesha kuwa nchi inaweza kufikia mafanikio makubwa zaidi katika soka.

Kauli hiyo inatokana na historia iliyowekwa na timu hiyo nchini Morocco kwa kufika fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza ingawa haikufanikiwa kuchukua taji ilishika nafasi ya pili baada ya kufungwa na Senegal katika mchezo wa fainali kwa mikwaju 4-2 ya penalti kufuatia sare tasa ndani ya dakika 90.

“Hakuna mtu aliyekuwa anaamini kama Tanzania tungefanya vizuri katika michuano ya AFCON, lakini kutokana na maandalizi mazuri yaliyofanywa na TFF kwa kuanzisha vituo vinavyozalisha vijana wenye vipaji vya kucheza mpira, tumeona mambo mengi yanawezekana,” amesema Nsangazelu.

Alieleza kuwa mafanikio hayo yanatoa matumaini makubwa kwa kizazi cha sasa na kijacho cha wachezaji wanaolelewa katika vituo hivyo, akisisitiza kuwa Tanzania ina nafasi ya kufikia viwango vya juu zaidi katika soka la vijana.

“Imetupa nguvu kuona hawa walioanza na wale ambao bado wapo vituoni. Kwa mwaka huu na miaka inayofuata tunaweza kuwa kwenye kiwango cha juu sana,” aliongeza.

Kocha huyo pia amewashukuru makocha wote waliohusika katika maandalizi ya timu hiyo kwa kujituma na kutekeleza majukumu yao kwa weledi hadi kuifikisha Serengeti Boys kwenye hatua iliyofikia.

Aidha, Nsangazelu ametoa wito kwa wadau wa soka nchini kuendelea kuwaunga mkono na kuwapa nafasi makocha wa ndani ili waweze kuchangia maendeleo ya mchezo huo.

“Tuendelee kutiana nguvu, hasa makocha wa ndani, ili tusaidie timu zetu ziweze kukua na kufikia mafanikio makubwa zaidi,” amesema.

Kauli ya Nsangazelu imekuja wakati Tanzania ikiendelea kupata pongezi kwa maendeleo ya soka la vijana, hatua inayotajwa kuwa msingi muhimu wa kujenga timu imara za taifa kwa siku zijazo.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button