Simba yamnasa Doumbia

DAR ES SALAAM: KLABU ya Simba imeendelea kuimarisha safu yake ya ushambuliaji baada ya kumtambulisha rasmi mshambuliaji raia wa Mali, Ibrahim Doumbia, kuelekea msimu mpya wa mashindano.
Doumbia, mwenye umri wa miaka 22, amejiunga na Wekundu wa Msimbazi akitokea klabu ya AS Kôrôfina ya Mali kwa mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza miaka miwili zaidi kulingana na makubaliano ya pande zote.
Mshambuliaji huyo anawasili Simba akiwa na rekodi nzuri ya kufumania nyavu baada ya kufunga mabao 21 katika msimu wa 2025/2026 akiwa na AS Kôrôfina, takwimu zinazotarajiwa kuongeza makali katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Doumbia pia anatarajiwa kujiunga moja kwa moja na kikosi cha Simba kinachoshiriki michuano ya CECAFA Kagame Cup 2026 inayofanyika jijini Kigali, Rwanda, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu mpya.
Usajili wa nyota huyo unaongeza chaguo kwa benchi la ufundi la Simba, ambalo linaendelea kukamilisha kikosi kitakachopambana katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho pamoja na mashindano ya kimataifa msimu huu.




