FANyumbani

Gomes aonya waamuzi fainali FA

KOCHA Mkuu wa Simba Didier Gomes, amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo wa fainali ya Kombe la FA dhidi ya watani zao Yanga, lakini amewataka waamuzi watakaochezesha mchezo huo kutenda haki  na siyo kupendelea upande mmoja.

Simba itavaana na Yanga katika mechi ya fainali ya FA, mchezo uliopangwa kupigwa Julai 25 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mpambano wa Ligi Kuu dhidi ya KMC ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 na kubakiza asilimia chache kutetea ubingwa wao, Gomes alisema hakufurahishwa na maamuzi ya Mwamuzi Emmanuel Mwandembwa kwenye mchezo wao uliopita wa ligi dhidi ya Yanga.

“Mwamuzi alitunyima penalti mbili za wazi kwenye mchezo dhidi ya Yanga, sasa hilo siyo jambo zuri huo ni mchezo wa fainali mwamuzi lazima awe makini na kuona matukio yote kwa usahihi ili mshindi apatikane kihalali,” alisema Gomes.

Kocha huyo alisema anajisikia furaha kufanikisha Simba kutetea ubingwa kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake na atajitahidi kukiimarisha vyema kikosi chake ili waendelee kufanya vizuri msimu ujao.

Alisema Simba kwa sasa ni timu kubwa Afrika hivyo nilazima iwe na utofauti katika mambo mengi ikiwemo usajili wake ili kuendelea kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa kama ilivyokuwa msimu huu ambapo walitolewa kwenye hatua ya robo fainali katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Namshukuru Mtendaji Mkuu Barbra Gonzalez amekuwa na msaada mkubwa kwangu katika kuimarisha timu lakini jana (juzi)  nilikuwa na kikao na Mwenyekiti wa Bodi Mohamed Dewji tumepanga mambo mazuri ambayo yataifanya Simba kuwa bora zaidi ya ilivyokuwa msimu huu,” alisema Gomes.

Aidha kocha huyo alisema baada ya kujihakikishia ubingwa amepanga kufanya mabadiliko katika mechi tatu zilizobaki kwa kuwapa nafasi wachezaji ambao hawakutumika kwa muda mrefu baadhi yao wakiwa ni Miraji Athumani, Gadiel Michael, Said Ndemla na David Kameta ‘Duchu’.

Alisema wachezaji hao wamekuwa na nidhamu ya hali ya juu kwa kipindi chote na anajisikia furaha kuwa sehemu ya kikosi cha Simba, ndio maana anataka kuwapa nafasi ili kuwapumzisha wengine ambao wametumika mfululizo kutokana na msimu kuwa mrefu pamoja na mechi 12 walizocheza za Ligi ya Mabingwa.

Related Articles

Back to top button