
DAR ES SALAAM: OFISA Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amewataka mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kutotarajia mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha kwanza kuelekea mchezo wa hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho CRDB dhidi ya Songea United.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Jumamosi, Machi 29, katika Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, jijini Dar es Salaam.
Kamwe amesisitiza kuwa wachezaji watakaopata nafasi ya kucheza ni wale pekee waliothibitisha ubora wao kwenye mazoezi na kumshawishi benchi la ufundi kuwa wanatosha kupewa majukumu katika mchezo huo muhimu.
“Hakuna muda wa kufumbia macho mapungufu wala kudharau mchezo wowote. Malengo yetu ni makubwa, na tunapaswa kuongeza umakini ili kuhakikisha tunafanikisha azma yetu,” amesema Kamwe.
Ameongeza kuwa Songea United inapaswa kutambua kwamba itakutana na Yanga yenye kiu ya kutetea ubingwa wake wa Kombe la Shirikisho CRDB.
“Tunawaambia ndugu zetu wa Songea kuwa wanakutana na Yanga ile ile ambayo wenzao waliikimbia Uwanja wa Benjamin Mkapa. Safari hii, wataikuta KMC Complex ikiwa imedhamiria kupambana kwa ushindi,” ameongeza.
Kuhusu hali ya kikosi, Kamwe amesema wachezaji wote walioko nje ya majukumu ya timu zao za taifa wako fiti na tayari kwa mchezo huo.
Aidha, nyota wa kikosi hicho, Yao Koussi, ameanza mazoezi binafsi na anatarajiwa kuungana na wenzake muda wowote.
Kwa ujumla, Yanga SC inatarajia kuingia uwanjani ikiwa na kikosi imara, chenye dhamira moja ya kuibuka na ushindi na kusonga mbele katika michuano hiyo.