Azam FC yamtambulisha Caleb Ilese

DAR ES SALAAM: Azam FC imeendelea kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu mpya wa mashindano baada ya kumtambulisha kiungo chipukizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Caleb Ilese, ambaye amekuzwa kupitia kituo cha kukuza vipaji cha klabu hiyo, Azam Academy.
Ilese anakuwa mchezaji wa nane kutambulishwa na Azam FC katika dirisha hili la usajili, hatua inayoonesha dhamira ya klabu hiyo ya kujenga kikosi imara kitakachowania mataji ya ndani na kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Kabla ya Ilese, Azam FC iliwatambulisha beki wa kushoto Taiwo Abdulrafiu kutoka Rivers United ya Nigeria, kiungo Donova Makoma kutoka Ufaransa, mshambuliaji John Mano kutoka Sudan, winga wa kimataifa wa Uganda Hassan Mubiru aliyesajiliwa kutoka SC Villa, pamoja na nyota wa DR Congo Henoc Moliq, Lupin Dieumerci na beki Henri Stanic.
Usajili huo unaonesha Azam FC imeamua kuchanganya wachezaji wenye uzoefu wa kimataifa na vipaji vilivyokuzwa ndani ya mfumo wake kupitia Azam Academy, ikiwa sehemu ya mkakati wa kuunda kikosi chenye ushindani mkubwa msimu ujao.
Mashabiki wa klabu hiyo sasa wanasubiri kuona kama safu hiyo mpya ya wachezaji itaifanya Azam FC kurejea kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kufanya vizuri katika mashindano mengine itakayoshiriki msimu huu.




