Ateba kuimarisha eneo la ushambuliaji Simba

DAR ES SALAAM: IKIWA imesalia siku moja kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili, klabu ya Simba iko mbioni kukamilisha usajili wa mshambuliaji kutoka USM Alger, Lepnel Ateba kwa ajili ya kuimarisha safu hiyo.
Hatua hiyo ni baada ya kufuata maagizo ya benchi la ufundi la timu hiyo inayoongozwa na Kocha Fadlu Davis baada ya kuona mapungufu ya kikosi chake kwenye safu ya ushambuliaji na kuwataka viongozi kuingia sokoni haraka.
Imeelezwa kuwa Simba imekamilisha uhamisho wa mshambuliaji huyo wa kimataifa raia wa Cameroon anayetarajia kusaini mkataba wa miaka miwili muda wowote kuanzia sasa wenye thamani ya sh million 542.
“Uongozi uliingia sokoni kuangalia aina ya mshambuliaji ambaye kocha (Fadlu) amependekeza na wamefanikiwa na wanazungumza na Ateba aliyewasili nchini jana kwa ajili ya mazungumzo hayo,” amesema mtoa habari huyo.
Ateba akisaini atachukua nafasi ya Freddy Michael ambaye atapelekwa kwa mkopo au kulipwa stahiki zake kabla ya dirisha la usajili kufungwa.
Kwa mujibu wa Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amewatazama wapinzani wote msimu huu anaiona timu yake ikifanya maajabu ya Dunia.
“Mpaka sasa Simba ndio timu yenye wachezaji bora wenye viwango vikubwa mno, kilichobaki ni kocha kutengeneza timu yenye mtiririko, muunganiko na maelewano ya pamoja.
Eneo pekee linalohotaji nguvu mpya ya nje ni eneo la ushambuliaji nalo viongozi wetu wanakamilisha mpango hivi punde,” amesema Ahmed.
Amesisitiza kuwa viongozi watakamilisha mahitaji ya kocha Fadlu baada ya kuona mapungufu ya timu hiyo kwa kupendekeza kusajiliwa mshambuliaji ambaye ataenda kuongeza nguvu .
“Wana Simba tuwe na subira tumpe nafasi Mwalimu wa kufanya kazi yake tutakapoanza kula matunda ya furaha kila mtu atapata tunda lake,” amesisitiza Ahamed.