La Liga

Barcelona yamng’oa Adeyemi Dortmund

BARCELONA: Mabingwa wa Hispania, Barcelona, wametangaza rasmi kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Ujerumani, Karim Adeyemi, kutoka Borussia Dortmund kwa ada inayokadiriwa kufikia euro milioni 29 (zaidi ya dola milioni 33 za Marekani) ikijumuisha malipo ya ziada kulingana na mafanikio yake.

Barcelona ilithibitisha kuwa Adeyemi amesaini mkataba wa miaka mitano utakaomuweka klabuni hapo hadi Juni 30, 2031, huku akiwa mchezaji wa pili kusajiliwa na klabu hiyo katika dirisha hili la usajili baada ya kiungo mshambuliaji wa England, Anthony Gordon, kutoka Newcastle United.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24 anatajwa kuwa nyongeza muhimu katika safu ya ushambuliaji ya Barcelona kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi mbalimbali, akiwa anaweza kucheza kama mshambuliaji wa kati au pembeni mwa uwanja.

Adeyemi anafahamika kwa kasi yake kubwa, uwezo wa kupenya kwenye ulinzi wa wapinzani na kumalizia nafasi, sifa ambazo Barcelona inatarajia zitasaidia kuongeza nguvu baada ya kuondoka kwa mshambuliaji mkongwe wa Poland, Robert Lewandowski.

Pia Barcelona ilipoteza huduma za Marcus Rashford baada ya kumalizika kwa kipindi chake cha mkopo kutoka Manchester United, hali iliyowaacha na hitaji la kuongeza nguvu mpya katika eneo la ushambuliaji.

Mbali na kumsajili Adeyemi, Barcelona bado inaendelea kumfuatilia mshambuliaji wa Atletico Madrid, Julian Alvarez, ambaye anaelezwa kuwa ndiye lengo lao kuu katika dirisha hili la usajili.

Ujio wa Adeyemi una historia maalumu na kocha wa Barcelona, Hansi Flick, ambaye ndiye aliyempa nafasi yake ya kwanza katika timu ya taifa ya Ujerumani mwaka 2021.

Adeyemi alijiunga na Borussia Dortmund mwaka 2022 akitokea Red Bull Salzburg, na katika kipindi chake cha misimu minne akiwa na klabu hiyo ya Ujerumani alifunga mabao 36 katika mechi 146 za mashindano yote kabla ya kuhamia Barcelona.

Barcelona inaamini ujio wa mshambuliaji huyo mwenye kasi utasaidia kuimarisha kikosi chake kinacholenga kutawala soka la Hispania na kufanya vizuri katika mashindano ya Ulaya msimu ujao.

Related Articles

Back to top button