Saliboko aweka rekodi mpya binafsi Scotland

SCOTLAND: Muogeleaji wa Tanzania, Collins Saliboko, ameendelea kuipeperusha vyema bendera ya taifa baada ya kuweka rekodi mpya binafsi katika mbio za mita 50 mtindo wa Backstroke kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola 2026 inayoendelea nchini Scotland.
Saliboko ametumia sekunde 28.31 katika mashindano yaliyofanyika leo, Julai 24, 2026, na kuvunja rekodi yake ya awali ya sekunde 28.88, hatua inayoonesha maendeleo makubwa ya kiwango chake katika mashindano ya kimataifa.
Akizungumza baada ya mbio hizo, Saliboko amesema ameridhishwa na mafanikio hayo na kueleza kuwa yataongeza ari ya kuendelea kufanya mazoezi kwa bidii ili kuboresha zaidi kiwango chake na kuiwakilisha Tanzania kwa mafanikio makubwa zaidi katika mashindano yajayo.
Mafanikio hayo yanakuja wakati ushindani ukiwa mkubwa kutoka kwa waogeleaji wa mataifa mbalimbali ya Jumuiya ya Madola, huku rekodi hiyo mpya ikiwa ishara ya maendeleo ya kuogelea nchini.
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limempongeza Saliboko kwa mafanikio hayo, likieleza kuwa rekodi mpya aliyoiweka ni matokeo ya juhudi, nidhamu na kujituma katika mazoezi.




