Kikosi Twinga Stars kambini Julai mosi
DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars), Bakari Shime ametangaza kikosi cha wachezaji 20, wanaotarajiwa kuingia kambini Julai Mosi, mwaka huu kujiandaa na michezo miwili ya kirafiki kama pasha pasha kuelekea michuano ya Fainalia ya Mataifa ya Afrika kwa wanawake (WAFCON).
Twiga Stars inatarajia kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Tunisia na Botswana ikiwa ni maandalizi ya michuano ya Fainalia ya Mataifa ya Afrika kwa wanawake (WAFCON) inayotarajia kufanyika Julai mwaka huu nchini Morocco.
Wachezaji hao ni Najat Abasi, Lidy Maximillian, Anastazia Katunzi, Joyce Lema, Stumai Athuman, Winfrida Geraid, (JKT Queens), Asha Mrisho (Aman Queens), Protasia Mbunda (Fountain Gate Princess), Enekia Kasonga (Eastern Flame, Saud Arabia), Juletha Singano (Juarez, Mexico).
Vailet Mwamakamba na Asha Juma (Simba Queens), Ester Maseke (Bunda Queens), Diana Lucas (Ame S.F.K, Uturuki), Maimuna Kaimu (ZED FC, Misri), Elizabert Charles (Alliance Girls), Aisha Masaka (BK Hacken, Sweden), Oppa Clament (Besiktas, Uturuki) na Clara Luvanga (Al Nasri, Saudi Arabia).
Akizungumza na Spotileo, Ofisa habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Clifold Ndimbo amesema wachezaji wote wanatarajia kuingia kambini kuanzia Julai Mosi, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Amesema kutokana na ligi za nchi mbalimbali kufikia tamati, wachezaji wengi wamerudi likizo hivyo wataingia kambini mapema kwa ajili ya mchezo huo ambao ni sehemu ya maandalizi ya michuano ya WAFCON.
“Leo tumetangaza kikosi cha wachezaji hao, baadae tutawajuza mechi hizo zitachezwa lini na wapinzani wetu wanatarajia kutua lini, taarifa zote hizo tutakuja kuziweka wazi baadae,” amesema Ndimbo.