Simba yaipania Galaxy kwao

KOCHA Mkuu wa Simba SC, Didier Gomes, amesema kuwa anaamini kikosi chake kitaendeleza walipoishia katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, watakaposhuka uwanjani Oktoba 17, kuwakabili Jwaneng Galaxy ya Botswana, kutafuta nafasi ya kuingia hatua ya makundi.
Simba inawafuata Galaxy, ambao wametinga hatua ya pili baada ya kuiondoa Diplomatic FC, kwa jumla ya mabao 2-1, ikianza kupata ushindi wa mabao 2-0 nyumbani kabla ya kwenda kupoteza 1-0 ugenini.

Simba iliishia hatua ya robo fainali iliposhiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika msimu wa mwaka 2020/21 baada ya kutolewa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, kwa jumla ya mabao 4-3.
Gomes, alisema kuwa anaamini utakuwa mchezo mgumu kutokana na tabia ya michezo ya Ligi ya Mabingwa, hasa
katika hatua ya mtoano kila timu inahitaji ushindi ili iweze kusonga mbele, lakini kwa maandalizi aliyoyafanya anaamini anaenda kushinda mjini Gaborone.
“Msimu huu malengo yetu ni makubwa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa tunahitaji kuendeleza pale tulipoishia tunataka kuvunja rekodi yetu ya msimu uliopita ya hatua ya robo fainali.”
“Tunawaheshimu wapinzani wetu wana timu nzuri, lakini sisi ni bora kuliko wao, nawaomba mashabiki na wapenzi wa Simba waendelee kuisapoti timu yao ili tuweze kutimiza kile tulichokipanga kwa msimu huu,” alisema Gomes.
Katika rekodi Simba misimu mitatu ya karibuni imefanikiwa kuingia hatua ya robo fainali mara mbili na kuiongezea pointi Tanzania, katika viwango vya ubora na kuifanya ipeleke timu nne katika mashindano ya Afrika, mbili Ligi ya Mabingwa na mbili Kombe la Shirikisho.