Nora Fatehi aunga mkono upingaji kuvuja mtihani India

MUMBAI: Mwigizaji na mwanamuziki maarufu Nora Fatehi ambaye amefanya remix ya wimbo wa ‘Pepeta’ wa msanii wa kitanzania Raymond maarufu Rayvan ametoa ujumbe wa kuunga mkono wanafunzi wanaoandamana nchini India kupinga madai ya uvujaji wa mitihani ya NEET, huku akieleza kusikitishwa na taarifa za baadhi ya wanafunzi kupoteza maisha kutokana na msongo wa mawazo.
Nora alitoa kauli hiyo kupitia ukurasa wake wa Instagram, siku mbili baada ya polisi wa Delhi kutumia nguvu kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakishiriki maandamano ya Chalo Sansad yaliyoandaliwa na kundi la Cockroach Janta Party (CJP).
Katika ujumbe wake, Nora alisema moyo wake uko pamoja na wanafunzi, familia zao na vijana wanaopitia kipindi kigumu kutokana na hali ya sintofahamu kuhusu mustakabali wao.
“Elimu ni zaidi ya mtihani au alama. Ni matumaini, ni kujitolea na ni ndoto ya kesho bora, si kwa mtu mmoja bali kwa taifa zima,” aliandika Nora.
Mwigizaji huyo alisema taarifa kuhusu madai ya uvujaji wa karatasi za mitihani zimewaacha wanafunzi wengi wakiwa wamechoka, wamevunjika moyo na kukata tamaa.
Alisema taarifa za baadhi ya wanafunzi kujitoa uhai zimemuathiri sana, akisisitiza kuwa hakuna mtihani, matokeo au mfumo wowote wa elimu unaopaswa kugharimu maisha ya kijana.
“Kwa familia zilizopoteza watoto wao, nawapa pole zangu za dhati. Maumivu mnayopitia hayawezi kuelezeka, na moyo wangu unaumia kwa ajili yenu,” alisema.
Katika ujumbe wake wa pamoja na picha aliyoweka, Nora aliwasifu wanafunzi wa India kwa ujasiri na uvumilivu wao, akisema aliamua kutumia jukwaa lake kuhamasisha uelewa na kuwataka wahusika kutafuta suluhisho la kudumu.
“Ninavutiwa na ujasiri wa wanafunzi nchini India. Naomba mfumo usimame pamoja na vijana ambao ndiyo mustakabali wa taifa,” aliandika.
Maandamano hayo yameendelea katika maeneo mbalimbali nchini India, huku wanafunzi, wazazi na waunga mkono wao wakitaka uwajibikaji na mageuzi katika mfumo wa mitihani.
Harakati hizo zinaongozwa na kundi la Cockroach Janta Party (CJP), lililoibuka baada ya kauli iliyodaiwa kutolewa na Jaji Mkuu wa India, Surya Kant, kuhusu wanaharakati vijana wasio na ajira, ambapo neno hilo liligeuzwa kuwa alama ya upinzani na mshikamano.
Miongoni mwa madai ya waandamanaji ni kutaka Waziri wa Elimu wa India, Dharmendra Pradhan, kujiuzulu pamoja na fidia ya rupia milioni 10 (takribani ₹1 crore) kwa familia za wanafunzi waliofariki kwa kujitoa uhai.
Mbali na Nora Fatehi, mastaa wengine wa India akiwemo Shabana Azmi, Prakash Raj, Sonakshi Sinha, Salman Khan, Alia Bhatt, Imran Khan na Rajkummar Rao wameonyesha kuunga mkono wanafunzi hao kupitia matamko mbalimbali.




