EPL

Anderson: Man City ni wafalme

....asajiliwa kwa fedha nyingi

MANCHESTER: Kiungo mpya wa Manchester City, Elliot Anderson, amesema hana shaka kuwa klabu hiyo ndiyo wafalme baada ya kukamilisha uhamisho wake kutoka Nottingham Forest kwa ada inayoripotiwa kufikia pauni milioni 116 (takribani Sh bilioni 420 za Tanzania).

City ilithibitisha Alhamisi kuwa kiungo huyo wa kimataifa wa England mwenye umri wa miaka 23 amesaini mkataba wa miaka mitano utakaomuweka Etihad hadi mwaka 2031, huku kukiwa na chaguo la kuongeza mwaka mmoja zaidi.

Anderson alisema amefurahia kutimiza ndoto ya kujiunga na moja ya klabu kubwa zaidi duniani, akieleza kuwa amevutiwa na utamaduni wa ushindi uliojengwa na Manchester City katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.

“Nimefurahi sana kujiunga na moja ya klabu kubwa duniani. Hii ni timu iliyojengwa kushinda mataji na kupambana katika kiwango cha juu kabisa. Hilo ndilo lililonivutia kuja hapa,” alisema Anderson.

Aliongeza kuwa mafanikio ya City katika miaka 10 hadi 12 iliyopita ndiyo yaliyomshawishi kuchagua kujiunga na mabingwa hao, akisema anatamani kuwa sehemu ya kikosi chenye kiu ya ushindi kila wakati.

Kiungo huyo pia ameonesha hamu kubwa ya kucheza dabi ya Manchester dhidi ya Manchester United, ambayo inatarajiwa kuchezwa Septemba 13 katika dimba la Old Trafford.

“Hii ni moja ya dabi kubwa zaidi duniani. Kwa muda wote ambao nimekuwa nikiifahamu Manchester, City wamekuwa wafalme wa jiji hili. Siwezi kusubiri kushiriki mechi hiyo,” alisema.

Anderson alianza soka lake katika akademi ya Newcastle United kabla ya kucheza mechi 55 za timu ya kwanza. Miaka miwili iliyopita alihamia Nottingham Forest kwa pauni milioni 35, ambako alicheza mechi 92 na kuvutia macho ya vigogo wa soka la England.

Msimu uliopita alipata mwito wake wa kwanza katika timu ya taifa ya England na kuwa sehemu muhimu ya kikosi cha kocha Thomas Tuchel kilichomaliza katika nafasi ya tatu kwenye Kombe la Dunia la FIFA 2026.
Licha ya hatua kubwa aliyofikia, Anderson amesema bado ana nafasi kubwa ya kuendelea kukua.
“Nina miaka 23 tu, hivyo bado nina muda mwingi wa kufikia kiwango changu bora. Bado sijafika nilipotaka kuwa, na naamini nina mengi zaidi ya kutoa uwanjani,” alisema.

Mkurugenzi wa soka wa Manchester City, Hugo Viana, amesema klabu hiyo inaamini Anderson ni mmoja wa viungo vijana wenye vipaji vikubwa duniani na ana uwezo wa kuwa kiungo kamili katika miaka ijayo.

Usajili wa Anderson unakuja siku chache baada ya kiungo mwenzake wa England, Morgan Rogers, kuhamia Chelsea kutoka Aston Villa kwa ada inayoripotiwa kufikia pauni milioni 117, iliyoweka rekodi mpya ya usajili wa mchezaji wa Uingereza.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button