Mama wa waigizaji wa filamu Casey na Ben Affleck afariki dunia

LOS ANGELES: Mama wa waigizaji wa filamu za mapigano maarufu wa Hollywood Ben Affleck na Casey Affleck, Chris Anne Boldt, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 83 baada ya kupambana na ugonjwa wa saratani ya kongosho kwa muda mrefu.
Familia ya Affleck ilitangaza kifo chake Julai 23, ikieleza kuwa Chris Anne alifariki Juni 2, miezi sita baada ya kugundulika kuwa na saratani hiyo mwezi Desemba 2025.
Ingawa taarifa rasmi ya chanzo cha kifo haikuwekwa wazi kwenye kumbukumbu ya mazishi, familia ilieleza kuwa baada ya kugunduliwa na ugonjwa huo, madaktari walimpa muda wa takribani miezi sita ya kuishi.
Chris Anne alizaliwa New York City mwezi Desemba 1942. Alikuwa mhitimu wa Chuo Kikuu cha Harvard na alitumia zaidi ya miaka 35 akifanya kazi kama mwalimu wa shule za umma.
Mbali na taaluma yake ya ualimu, Chris Anne alikuwa mwanaharakati wa haki za kiraia na alishiriki katika harakati za Freedom Riders miaka ya 1960 zilizolenga kupinga ubaguzi wa rangi nchini Marekani.
Akiwa na mume wake wa zamani Timothy Affleck, walimkaribisha duniani Ben Affleck mwaka 1972, kabla ya kupata mtoto mwingine, Casey Affleck, mwaka 1975. Familia hiyo baadaye ilihamia Massachusetts ambako Chris Anne aliendelea na kazi yake ya ualimu.
Ben Affleck amewahi kueleza kuwa mama yake alikuwa na mchango mkubwa katika maisha yake na mafanikio yake ya Hollywood. Chris Anne alitumia uhusiano wake na rafiki yake wa zamani, Patty Collins, aliyekuwa mkurugenzi wa waigizaji, kumsaidia Ben kupata nafasi za kwanza katika matangazo na filamu za televisheni.
Chris Anne aliendelea kuwa mshauri na msaidizi mkubwa kwa watoto wake wawili katika safari yao ya uigizaji. Alisindikiza Ben katika hafla ya tuzo za Oscar mwaka 1998 ambapo Ben na Matt Damon walishinda tuzo ya Oscar kupitia filamu ya Good Will Hunting, ambayo pia ilimshirikisha Casey Affleck.
Chris Anne ameacha watoto wawili, Ben na Casey Affleck, pamoja na wajukuu watano akiwemo Violet, Fin na Sam wa Ben, pamoja na Atticus na Indiana wa Casey.




