Mastaa

Steve Nyerere: Mainda alitulisha wakati tunajitafuta

DAR ES SALAAM: MSANII wa filamu nchini, Steve Nyerere, amemkumbuka mwigizaji mwenzake Mainda kwa msaada mkubwa aliompatia katika kipindi cha mwanzo wa safari yake ya kisanii, wakati alipokuwa akikabiliwa na changamoto za maisha.

Steve amesema kuwa enzi hizo yeye na baadhi ya wasanii wenzake walikuwa hawana uwezo wa kujikimu, lakini Mainda aliwafungulia milango ya nyumbani kwake na kuwakaribisha kwa chakula, akiwalisha ugali, dagaa na matembele, jambo ambalo liliwapa faraja na nguvu ya kuendelea kupambana.

Kupitia ukurasa wake rasmi wa Instagram, Steve ameeleza kuwa mbali na kuwapatia chakula, Mainda aliwahi pia kuwasaidia fedha za nauli na hata kuwaambia wafike nyumbani kwake mapema siku inayofuata kwa kuwa angekuwa nyumbani siku nzima.

Amesimulia kuwa siku iliyofuata aliwasili nyumbani kwa Mainda majira ya saa tatu asubuhi, lakini alipofika alimkuta bado hajaamka.

Hivyo, amelazimika kusubiri nje ya nyumba hiyo huku mpangaji mmoja akimkaribisha chai na vitumbua.

Steve amesema wakati Mainda alipoamka na kutoka nje, alimkuta akiwa tayari anakula kitumbua cha tano, jambo ambalo liliibua kicheko na kubaki kuwa moja ya kumbukumbu za kipekee katika maisha yake.

Amehitimisha simulizi hilo, Steve alimshukuru Mainda kwa moyo wake wa upendo na ukarimu, akisisitiza kuwa amekuwa na nafasi ya pekee maishani mwake na humchukulia kama dada yake.

Steve Nyerere na Mainda ni miongoni mwa wasanii wa kizazi cha mwanzo cha filamu za Kitanzania walioanza kung’ara mwanzoni mwa miaka ya 2000 na baadaye kujizolea umaarufu mkubwa katika tasnia ya filamu nchini.

Related Articles

Back to top button