Mr Beast atoa misaada Kenya

NAROK:MWANAYOUTUBE maarufu kutoka Marekani, MrBeast, amekuwa gumzo nchini Kenya baada ya kutoa misaada mbalimbali katika Kaunti ya Narok.
MrBeast, ambaye jina lake halisi ni James Stephen Donaldson, ni mfanyabiashara na mfadhili maarufu. Alifika katika Shule ya Msingi ya Oloirien, ambapo alianza kwa kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kutoa nyenzo za kilimo kwa jamii inayozunguka shule hiyo.
Katika video yake ya Aprili 12, MrBeast alionekana akiwa na timu yake shuleni hapo, akiahidi kulisha watu wengi kadri video hiyo itakavyopata maoni.
“Ukitazama video hii, utasaidia kusambaza mashamba, kujenga jiko kubwa, kujenga shule na kutoa chakula kwa wanafunzi, na kuokoa watoto dhidi ya ajira za utotoni,” alisema.
Alisema kuwa kupitia programu yao ya chakula, mahudhurio ya wanafunzi shuleni hapo yameongezeka kwa kiwango kikubwa.
MrBeast na timu yake walinunua madawati mapya kwa ajili ya wanafunzi waliokuwa wakikaa chini. Ili kuendeleza mpango wa chakula, jamii inayozunguka shule hiyo ilipewa teknolojia ya kisasa ya kilimo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji.
Alinunua trekta kwa ajili ya shamba linaloendeshwa chini ya misingi yake. Shamba hilo limegawanywa sehemu mbalimbali, ambapo kipande kimoja kinatumika kwa uzalishaji wa chakula cha shule.
Mbali na hilo, alitoa lori kwa ajili ya kusambaza mazao ya ziada sokoni, na pia alijenga jiko jipya, kubwa na la kisasa ili kuwezesha utoaji wa milo miwili kwa siku kwa wanafunzi.
Kisima, tanki la kuhifadhia maji, chafu na shamba pia vilijengwa ili kuhakikisha kuwa shule hiyo haikosi chakula.
MrBeast hutangaza shughuli zake za misaada kupitia akaunti yake ya YouTube ambayo ina zaidi ya wanachama milioni 380.