Muziki

Toxic Lyrikal: Sikutaka kwenda kutumbuiza Ikulu

NAIROBI: RAPA maarufu kutoka Kayole, Nairobi nchini Kenya, Timothy Omondi maarufu Toxic Lyrikali amewaacha wengi wakishangaa baada ya kudai kwamba hakuwahi kuwa na mpango wa kuhudhuria hafla iliyofanyika Ikulu ya Nairobi Kenya licha ya kualikuwa kutumbuiza.

Akizungumza katika mahojiano yaliyosambazwa mtandaoni, msanii huyo amesema awali alikataa mwaliko huo mara kadhaa na aliamua kutokwenda kabisa.

Kwa mujibu wa Toxic Lyrikali, mazungumzo yaliendelea nyuma ya pazia kati ya waandaaji wa hafla hiyo na timu yake ya usimamizi hadi kufikia hatua ya yeye kuingizwa rasmi kwenye ratiba ya tukio hilo.

Rapa huyo amesema hata siku ya tukio alipokuwa akiandaliwa kwenda bado hakuwa na hamasa yoyote ya kushiriki. Alieleza kuwa alikuwa ametoka kuamka na ghafla akaambiwa anatakiwa kuondoka haraka kuelekea kwenye hafla hiyo.
“Sikutaka kwenda ‘State House’ kabisa,” alikiri msanii huyo huku akieleza kuwa safari nzima aliendelea kulalamika na kuhoji kwa nini alihudhuria.

Toxic amesema alikuwa anatamani kubaki mtaani kwake na kutumia siku hiyo kwa utulivu badala ya kuhudhuria hafla hiyo ya kitaifa.

Hata hivyo, mambo yalibadilika baada ya kupewa uhakika kuwa ziara hiyo isingechukua muda mrefu. Aliambiwa angeenda kumsalimia Rais kisha kurejea nyumbani.

Mwisho wa siku, rapa huyo aliamua kuachana na msimamo wake wa awali na kwenda kuhudhuria hafla hiyo.

Kauli zake zimeibua mjadala mkubwa mitandaoni, huku baadhi ya mashabiki wakimsifu kwa kusema ukweli wake na wengine wakishangazwa na namna alivyosuasua kabla ya kuhudhuria tukio hilo muhimu.

Related Articles

Back to top button