Netflix kuachia filamu ya Michael Jackson, Lukas Podolsk mwezi huu

LOS ANGELES: JUKWAA kubwa la utazamaji duniani, Netflix, limewaandalia mashabiki wake mwezi wenye pilika nyingi baada ya kutangaza ujio wa makala nane mpya zitakazoanza kuoneshwa mwezi huu wa Juni 2026.
Miongoni mwa kazi hizo zinazovutia zaidi ni makala inayomhusu nyota wa zamani wa soka la Ujerumani, Lukas Podolski, inayojulikana kwa jina la ‘Poldi’.
Makala hiyo itafungua pazia la maisha ya mshambuliaji huyo ndani na nje ya uwanja, ikionesha safari yake kama mchezaji, mfanyabiashara na shujaa wa jamii.
Kwa mashabiki wa matukio ya kweli ya uhalifu, Netflix imeandaa ‘The Murder of Rachel Nickell’, makala inayochunguza mauaji yaliyotikisa Uingereza mwaka 1992 na jinsi uchunguzi wa polisi ulivyozua maswali mengi kwa miaka kadhaa.
Wapenzi wa soka nao hawajasahaulika. Makala ya ‘USA 94: Brazil’s Return to Glory’ itarejesha kumbukumbu za safari ya Brazil kuelekea ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 1994, moja ya mafanikio makubwa katika historia ya soka duniani.
Katika upande wa historia, Netflix itazindua ‘The American Experiment’, mfululizo wa vipindi vitano vinavyochunguza historia ya Marekani tangu mapinduzi ya uhuru hadi kuzaliwa kwa katiba ya taifa hilo.
Lakini kazi inayovuta hisia zaidi ni ‘Michael Jackson: The Verdict’, makala maalum ya sehemu tatu inayorejea moja ya kesi zilizotikisa ulimwengu wa burudani na maisha ya mfalme wa muziki wa Pop, Michael Jackson.
Badala ya kuangazia mafanikio yake ya muziki pekee, makala hiyo itachunguza kwa kina tuhuma za unyanyasaji wa watoto zilizowahi kumkabili pamoja na uamuzi wa mahakama uliomkuta hana hatia mwaka 2005.
Netflix inaonekana kuendelea kuwekeza katika maudhui ya kweli yanayogusa michezo, historia, uhalifu na maisha ya watu maarufu, jambo ambalo limeifanya kuwa moja ya majukwaa yanayoongoza katika utayarishaji wa makala duniani.
Kwa mashabiki wa simulizi za kweli, Juni inaonekana kuwa mwezi wa kukaa mbele ya skrini kwa muda mrefu, huku kila wiki ikiahidi hadithi mpya za kusisimua kutoka pembe mbalimbali za dunia.
Kuanzia maisha ya Lukas Podolski, historia ya Brazil ya mwaka 1994 hadi simulizi tata ya Michael Jackson, Netflix imeweka mezani menu nzito ambayo huenda ikawa gumzo kubwa la mwezi huu wa Juni.




