Mwanamaudhui wa Kenya Tabitha Gatwiri afariki ghafla
MTAYARISHAJI wa maudhui ya mtandaoni Tabitha Gatwiri amefariki dunia na kuacha pengo katika jamii ya wabunifu nchini Kenya.
Kulingana na ripoti iliyotolewa leo, Gatwiri, anayejulikana kwa uchekeshaji wake mahiri katika safu zake mbalimbali ikiwemo TikTok, ameugua ghafla hadi mauti yalipomkuta.
Mwili wake ulipatikana katika makazi yake, na polisi wameanza uchunguzi kuhusu kifo chake cha ghafla, huku wakibainisha kuwa hivi karibuni alikuwa na wasiwasi kuhusu afya yake.
Mwili wa Gatwiri umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kenyatta.
Kifo chake kimeibua huzuni miongoni mwa waandaaji wenzake wa maudhui mitandaoni, mashabiki wake na wadau mbalimbali wa mahudhui yake huku wengi wao wakisambaziana habari kuhusu kifo hicho cha ghafla.
Msichana huyo mwenye miaka 29 alipata umaarufu nchini Kenya baada ya kutoa maudhui kuhusu ‘Mpenzi wa Chuo Kikuu’ huku akionesha jinsi mapenzi yanavyotiwa chumvi wakati yanaanza.
Hata hivyo licha ya wengi kudhani kwamba kipande hicho kilihusu uhalisia wake, baadae alitolea maelezo ya kukanusha kwamba kilikuwa ni tukio la kubuni lililokuwa na lengo la kuelimisha na kuchekesha tu.