Filamu

Rambo arejea arekodi filamu yake nchini Thailand

THAILAND: MASHABIKI wa filamu za mapigano wana sababu ya kutabasamu baada ya taarifa kuthibitisha kuwa filamu mpya ya John Rambo imeanza rasmi kurekodiwa nchini Thailand, huku muigizaji Noah Centineo akitarajiwa kuvaa viatu vya gwiji wa movie za mapigano Sylvester Stallone kwa mara ya kwanza.

Kampuni ya Lionsgate imetangaza kuwa uzalishaji wa filamu hiyo mpya umeanza katika maeneo mbalimbali ya Thailand, ikiwemo Bangkok, Krabi, Phang Nga na Kanchanaburi.

Filamu hiyo itakuwa ikisimulia maisha ya John Rambo kabla ya matukio ya filamu maarufu ya ‘First Blood’ iliyotoka mwaka 1982.

Kwa miaka mingi, jina la Rambo limekuwa sawa na ujasiri, mapambano na vita visivyo na huruma. Safari hii, mashabiki watapata nafasi ya kuona mwanzo wa hadithi ya shujaa huyo kabla hajawa askari mgumu anayejulikana duniani kote.

Jambo lililovuta hisia zaidi ni uamuzi wa kumpa Noah Centineo jukumu la kuigiza John Rambo kijana. Nyota huyo anayefahamika kupitia filamu mbalimbali za Hollywood sasa anakabiliwa na kazi kubwa ya kurithi nafasi iliyomjengea umaarufu mkubwa Sylvester
Stallone kwa zaidi ya miongo minne.

Filamu hiyo inaongozwa na Jalmari Helander, mtayarishaji aliyepata sifa kupitia filamu ya Sisu, huku Rory Haines na Sohrab Noshirvani wakihusika katika uandishi wa hadithi.

Mbali na Stallone kuendelea kuwa sehemu ya mradi huo kama mtayarishaji mtendaji, ndugu maarufu Anthony Russo na Joe Russo nao wameungana katika timu ya watayarishaji wa filamu hiyo.

Thailand imekuwa sehemu muhimu katika historia ya filamu za Rambo kwa miaka mingi, jambo ambalo limeifanya kurejea tena kuwa sehemu ya simulizi mpya ya shujaa huyo wa vita.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, filamu hiyo inatarajiwa kuingia rasmi kwenye kumbi za sinema mwaka 2027 na tayari imeanza kuamsha hamasa kubwa miongoni mwa mashabiki wa filamu za mapigano duniani.

Related Articles

Back to top button