Mastaa

Akshay Kumar auza nyumba zake mbili zaidi ya bilioni 2

MUMBAI: NYOTA wa Bollywood, Akshay Kumar, ameendelea kuonesha kuwa mbali na mafanikio ya filamu, pia ni bingwa wa uwekezaji baada ya kuuza nyumba zake mbili zilizopo katika jiji la Mumbai nchini India ambapo ameziuza kwa mamilioni ya fedha.

Ripoti za mali isiyohamishika nchini India zinaeleza kuwa muigizaji huyo ameuza nyumba zake mbili zilizopo katika jengo la kifahari la Oberoi Sky City eneo la Borivali kwa jumla ya rupia crore 7.1 ambazo ni zaidi ya bilioni 2.

Nyumba kubwa zaidi kati ya hizo iliuzwa kwa rupia crore 5.75 huku nyingine ikiuzwa kwa rupia crore 1.35, hatua iliyomwingizia faida kubwa kutokana na uwekezaji alioufanya miaka kadhaa iliyopita.

Akshay alinunua nyumba hizo mwaka 2017 kwa gharama ndogo zaidi ikilinganishwa na thamani yake ya sasa, jambo linaloonesha namna soko la nyumba lilivyokua kwa kipindi hicho.

Taarifa zinaeleza kuwa mnunuzi wa nyumba hizo ni mfanyabiashara mmoja aliyezikamilisha rasmi kupitia usajili wa Juni 2, 2026.

Kwa miaka ya karibuni, Akshay amekuwa akijulikana si tu kwa mafanikio yake kwenye filamu bali pia kwa uwekezaji wake mkubwa katika sekta ya mali isiyohamishika.

Wachambuzi wa biashara nchini India wanaamini kuwa nyota huyo amepata faida kubwa kutokana na ongezeko la thamani ya mali zake ndani ya kipindi cha karibu miaka nane.

Related Articles

Back to top button