Kuogelea

BMT yawataka waogeleaji kurejea na medali Mauritius

DAR ES SALAAM:BARAZA la Michezo la Taifa (BMT) limewataka waogeleaji wa Tanzania wanaoshiriki Mashindano ya Kuogelea ya Wazi ya Afrika nchini Mauritius kurejea nyumbani na medali, likisisitiza kuwa safari yao si ya kushiriki tu bali ni ya kushindana na kuiletea nchi heshima.

Ofisa Michezo Mwandamizi wa BMT, Ingrid Kimario, alitoa kauli hiyo wakati wa kuiaga timu ya taifa ya waogeleaji ya Open Water iliyoondoka alfajiri ya leo kuelekea Mauritius kushiriki mashindano hayo yatakayofanyika Juni 6 na 7 mwaka huu.

“Hatua mliyofikia ni ya kupongezwa na inatia moyo. Tunaamini hamuendi kushiriki tu, bali mnakwenda kushindana na kuiletea Tanzania ushindi. BMT ipo pamoja nanyi na tunatarajia kuona medali nyingi zikirejea nyumbani,” amesema Kimario.

Waogeleaji hao ni Adil Abdurahman, Ethan Makalla, Kabeer Lakhan na Lolita Borega.

Kwa upande wake, Katibu wa Kamati ya Open Water chini ya Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Ramadhan Namkoveka, amesema maendeleo ya mchezo huo nchini yanaendelea kuimarika kutokana na juhudi za chama hicho katika kukuza vipaji vya waogeleaji.

Amesema mwaka jana TSA ilifanikiwa kuandaa mashindano ya taifa yaliyowezesha baadhi ya vijana kupata nafasi ya kushiriki mashindano yaliyofanyika Mombasa, Kenya, hatua iliyochangia kuongeza uzoefu kwa waogeleaji wa Tanzania.

Namkoveka amesema safari hii Tanzania itawakilishwa na waogeleaji hao wanne watakaoshiriki katika mbio za kilometa tano, kilometa tatu, mita 1,500, mita 1,000 na mita 500 za mtoano.

“Kwa sasa bado tuna idadi ndogo ya washiriki wa mchezo huu nchini, lakini tunaendelea kufanya jitihada za kuhamasisha vijana wengi zaidi kujitokeza na kushiriki Open Water,” amesema.

Kocha wa timu hiyo, Khalid Rushaka, amesema maandalizi ya wachezaji yamekuwa mazuri na kwamba wamepata uzoefu wa kutosha kupitia ushiriki wao katika mashindano mbalimbali ya kimataifa yaliyofanyika Kenya na Algeria.

Naye Katibu Mkuu wa TSA, Inviolata Itatiro, aliipongeza Kamati ya Open Water kwa juhudi zake za kuendeleza mchezo huo na kufanikisha ushiriki wa timu katika mashindano ya Mauritius.

“Tuna matarajio makubwa kwa timu yetu. Tunaamini wachezaji wetu watafanya vizuri na kuliletea taifa heshima,” amesema Itatiro.

Related Articles

Back to top button