Mitindo

Makonda: Tuhubiri amani na kumtanguliza Mungu kwenye saluni zetu

.....tuache ushirikina

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amewataka wamiliki na wafanyakazi wa saluni nchini kumtanguliza Mungu katika shughuli zao za kila siku, akisisitiza kuwa mafanikio ya kweli yanatokana na kipaji alichowapa Mungu na si ushirikina.

Makonda amesema kuwa tangu amelipopewa dhamana ya uwaziri ameendelea kumtanguliza Mungu, akieleza kuwa kufanya hivyo kumemfungulia milango ya mafanikio.

Amewahimiza watu wanaofanya kazi katika saluni kutomuacha Mungu na kuachana na imani za ushirikina.

“Ukimtanguliza Mungu, milango mingi itafunguka kupitia kipaji cha mikono yako. Nikiwa Waziri sijamuacha Mungu, wala sitamuacha. Ninyi watu wa saluni msimwache Mungu; acheni ushirikina, mwombeni Mungu,” amesema Makonda.

Aidha, amesema ni muhimu saluni ziwe sehemu za kuhubiri amani, ili wafanyakazi waweze kutekeleza shughuli zao kwa uhuru, usalama na kujipatia kipato cha halali.

Makonda pia ametoa wito kwa wananchi kuepuka kuwahukumu watu kwa kuangalia mafanikio yao ya nje pekee.

Amesema mara nyingi watu huwatamani wenzao wanaoonekana kuwa na maisha mazuri, bila kujua changamoto wanazopitia.

“Unaweza kumwona dada akiendesha gari zuri ukatamani ungekuwa wewe, lakini hujui maumivu au changamoto anazopitia. Wakati mwingine anatamani hata amani aliyonayo mtu wa kawaida,” amesema.

Related Articles

Back to top button