Mitindo

Magese jaji mkuu Samia Fashion Festival

MWANAMITINDO wa Kimataifa, Mellen Magese ametangazwa kuwa Jaji Mkuu wa Tamasha la Samia Fashion Festival litakalofanyika Novemba 30 mwaka huu visiwani Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutangazwa kuwa Jaji mkuu wa tamasha hilo , Magese amesema kuwa ni heshima kubwa na furaha kwake kusimama kama Jaji Mkuu wa Samia Fashion Festival na kwamba anajivunia kushuhudia wakati huu wa kihistoria ambao unasherehekea ubunifu, stara, na urithi wa kipekee wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

Amesema walioteuliwa kuwa majaji wanaamini kuwa tukio hili ni kubwa na litakalobakia katika kumbukumbu kwa miaka mingi ijayo.

“Kwa zaidi ya miaka ishirini, nimejitolea maisha yangu katika sekta ya mitindo, urembo. Nimezunguka duniani, nikifanya kazi na chapa kubwa na maarufu, nimeona jinsi mitindo inavyothaminiwa katika nchi za Ulaya na mataifa mengine, si tu kama sanaa bali kama alama ya utambulisho, urithi, na fahari.

“Niliposikia kuhusu mpango huu wa kipekee, sikusita, nilichukua ndege haraka kuja nyumbani kuwa sehemu ya safari hii ya kihistoria, kwa tamasha hili si tu kuhusu mavazi; ni kuhusu heshima yetu kama Watanzania,”amesema.

Mrembo huyo ambaye anaishi nchini Marekani kwa sasa amesema uandaaji wa Vazi la Samia alama ya stara, uongozi, na heshima ni zaidi ya mavazi ya kawaida. Ni kazi ya sanaa inayostahili kuhifadhiwa katika makumbusho kwa vizazi vijavyo, kama heshima kwa urithi wa kiongozi huyo.

Ameeleza ilikuwa ni ndoto yake ya siku nyingi kuona Vazi la Samia linakuwa ishara ya kitaifa na kimataifa, chanzo cha fahari kinachowakilisha uzuri, nguvu, na umoja wa Tanzania.

“Tukubaliane kufanya kitu cha kipekee, kitu kitakachotupeleka ulimwenguni na kuacha alama katika historia.

Kwa wabunifu, wanamitindo, na wote wanaoshiriki, tambueni kuwa hampo tu katika sehemu ya tamasha, bali mnakuwa sehemu ya historia ya kizazi kitakachovutia dunia. Hebu tufanye wakati huu uwe wa kukumbukwa milele.”

Awali akizungumza kuhusu Samia Fashion Festival Mwanzilishi na Muandaaji wa Tamasha hilo Khadija Mwanamboka amesema amewashirikisha wanamitindo mbalimbali na kuungana nao katika tamasha hilo ili kusaidia watoto wanaoishi na virusi vya UKIMWI na Saratani.

Kwa upande wa Mwigizaji maarufu nchini, İdris Sultan amesema anajisikia furaha kuwa sehemu ya walioshirikishwa katika eneo la majaji na kueleza umefika wakati kwa Watanzania kutoa nafasi kwa wanawake wenye uwezo ukiwemo uongozi na kusisitiza Rais Samia amekuwa mfano mzuri na wa kuigwa .

Related Articles

Back to top button