
KOCHA Mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Kim Poulsen amesema amefurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na timu yake na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0, huku wakijifunza mengi kutoka kwa wapinzano wao hao.
Stars juzi iliibuka na ushindi huo katika mchezo wa kusaka tiketi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia kwenye Uwanja wa Leopold Sedar Senghor, Benin.
Ushindi huo umeifanya Tanzania irejee kileleni mwa Kundi J ikiwa na pointi saba sawa na Benin, huku timu hizo zikipishana kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa baada ya michezo minne.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Poulsen alisema kuwa katika michezo miwili waliyokutana na Benin wamejifunza mengi.
“Nina furaha sana baada ya kupata matokeo haya ya ushindi tulicheza vizuri nchini Tanzania, lakini tukashindwa kupata ushindi.
“Leo (juzi) tulikuwa na mchezo mgumu dhidi ya Benin, lakini kutokana na somo tulilopata kutoka katika mchezo wa mwanzo, imetusaidia.
“Baada ya mchezo wa kwanza tulijua staili yao ya uchezaji tukabadili kidogo aina ya uchezaji wetu, lakini pia tukatumia ubora wetu kupata matokeo,” alisema Poulsen.
Poulsen alisema kuwa jana (juzi) wamekuwa na furaha tofauti na siku tatu zilizopita, ambapo walikuwa na huzuni baada ya kupoteza katika ardhi ya nyumbani.
Alisema kuwa hivi sasa nguvu anazihamishia katika mchezo ujao dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) utakaochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, kabla ya kumaliza michezo ya makundi ugenini dhidi ya Madagascar.