Ligi Kuu

Yanga yatwaa ubingwa kwa rekodi, Mtibwa yashuka daraja

DAR ES SALAAM:YANGA imehitimisha msimu wa Ligi Kuu Bara kwa kishindo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo wa mwisho uliochezwa Uwanja wa Jenerali Isamuhyo, na kutwaa ubingwa kwa mara ya tano mfululizo huku ikiweka rekodi ya kufikisha pointi 75, idadi ambayo haijafikiwa na timu yoyote msimu huu.

Ubingwa huo ni wa 31 kwa klabu hiyo na wa tano mfululizo tangu kuingia kwa mwekezaji Ghalib Said Mohamed, huku ukipatikana chini ya uongozi wa Rais wa klabu, Hersi Said.

Yanga ilipata mabao yake kupitia kwa Prince Dube, Maxi Nzengeli na Laurindo Aurelio ‘Depu’, yaliyoihakikishia kumaliza msimu kwa kishindo mbele ya mashabiki wake.

Mchezo huo pia ulikuwa na tukio la kusikitisha baada ya beki wa JKT Tanzania, Hassan Twalib, kupewa kadi nyekundu dakika ya 45 kwa kumchezea vibaya Pacome Zouzoua, ambaye alilazimika kutolewa nje ya uwanja kwa machela kutokana na majeraha aliyoyapata.

Katika michezo mingine ya mwisho wa msimu, Simba iliifunga KMC bao 1-0 lililowekwa wavuni na Inno Loemba, huku Azam FC ikishinda mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji.

Fountain Gate iliibuka na ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Singida Black Stars, Mashujaa ikifungwa bao 1-0 na Tanzania Prisons, Namungo ikaifunga Mtibwa Sugar mabao 2-1, Coastal Union ikaibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Pamba, huku Mbeya City na TRA zikitoshana nguvu kwa sare ya 0-0.

Matokeo hayo yameifanya Mtibwa Sugar kuungana na KMC kushuka daraja baada ya kumaliza nafasi ya 15 ikiwa na pointi 27.

Kwa upande mwingine, Mbeya City na Tanzania Prisons zimemaliza katika nafasi za mtoano na sasa zitapambana kutetea nafasi zao za kubaki Ligi Kuu msimu ujao.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button