Nyumbani

Makonda awataka wasusi na vinyozi kujiendeleza kielimu kukuza biashara zao

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amewataka wasusi na vinyozi nchini kujiendeleza kielimu ili kuongeza ujuzi na kukuza biashara zao kwa kutoa huduma zenye viwango vya juu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Chama cha Salonist Tanzania, Makonda amesema taaluma ya ususi na unyoaji ina nafasi kubwa ya kuchangia uchumi, hivyo ni muhimu kwa wahudumu wa saluni kuzingatia maadili na huduma bora kwa wateja.

Amewataka wasusi kuacha tabia ya kuwazungumzia watu wanapokuwa katika maeneo ya kazi na badala yake wajikite katika kuwahudumia wateja kwa heshima, weledi na usiri.

“Pindi mteja anapokuja saluni, mhudumieni kwa umakini. Muwe na nidhamu ya kazi na muache kuwajadili watu ofisini kwenu. Wekeni kufuli midomoni,” amesema Makonda.

Aidha, amewashauri kujifunza namna bora ya kumshauri mteja kulingana na mahitaji yake, kupanga muda wa kazi na mapumziko ili kulinda afya zao na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

Makonda pia amewataka kuwa waaminifu kwa wateja kuhusu bidhaa wanazotumia na kuziuza, akisisitiza kuwa lengo liwe kuwafanya wateja wapendeze badala ya kutafuta faida kwa kuwapa bidhaa zisizofaa.

“Mwelezeni mteja ukweli kuhusu bidhaa. Msifanye hivyo kwa lengo la kupata fedha pekee, bali hakikisheni mnamsaidia apate huduma bora na mwonekano mzuri,” amesema.

Vilevile, amehimiza uzalishaji wa bidhaa za urembo zinazotengenezwa nchini ili kuongeza thamani ya bidhaa za Tanzania na kufungua masoko ya ndani na nje ya nchi.

“Tutengeneze bidhaa zetu ili tuweze kuziuza ndani na nje ya Tanzania,” amesisitiza Makonda.

Related Articles

Back to top button