MastaaMitindo

ANNASTAZIA CHARLES: Msichana mdogo anayetoa jasho wakubwa

MAISHA yana mengi ya kujifunza lakini zaidi ya hayo uthubutu na kujituma ni njia mojawapo ya kukomboa vijana hususani mwanamke katika jamii.

Vijana hasa wa kike wanaweza kupata ukombozi huo wa kiuchumi kutokana na elimu, ujuzi na stadi za kazi na weledi wao. Eneo hili likizingatiwa ni mtaji wa uhakika kwa vijana nchini kuwawezesha ama waweze kujiajiri au kuajiriwa.

Miongoni mwa vijana wa kike wanufaika na waliotumia vyema elimu , ujuzi na stadi za kazi ni Annastazia Charles (23) ambaye ni mzaliwa wa kijiji cha Senga , wilaya ya Geita na mkoa wa Geita.

Annastazia(Anna),ni mhitimu wa fani ya usimamizi majengo na barabara aliyoisomea nyakati hizo katika Chuo cha Ufundi Mbeya (MTC), sasa ni Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia( MUST).

Anasema alijiunga kusomea masuala ya usimamizi majengon a barabara katika Chuo hicho baada ya kufanya vizuri masomo yake ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Good Will inayomilikiwa na kanisa la Adventst mkoani Shinyanga.

Annastazia anasema baada ya kumaliza chuo alipata kazi katika kampuni aliyoitaja kwa kifupi CFB Ltd ya kusimamia ujenzi wa majengo ya Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)wilayani Chato , mkoani Geita.

Kampuni hiyo pia ilimpeleka katika jiji la Mwanza kusimamia ujenzi wa majengo ya vyoo vya shule moja ya msingi jijini humo. Annastazia anasema alitoka Mwanza hadi mkoani Morogoro baada ya kumalizana na kampuni hiyo na alifanikiwa pia kupata kazi kwenye kampuni binafsi akiwa Morogoro.

Kazi hiyo ilikuwa pia ya kusimamia ujenzi wa jengo la ghorofa mbili la hosteli ya wanafuzi Chuo cha Mafunzo ya Mifugo (LITI). Anasema msimamizi wa miradi ya ujenzi anahusika kubuni na kujenga miradi ya ujenzi kwa kufuata vigezo na michoro ya ramani za majengo hayo.

Annastazia anasema suala la kazi kwake amelipa kipaumbele cha juu na kwamba yupo makini katika kazi zake za usimamizi wa ujenzi wa majengo mbalimbali.

“Hakuna kitu kinachonishinda kusimamia linapokuja suala la ujenzi wa majengo, kwani nafuata vipimo na michoro kwenye karatasi na kuiweka kwenye utekelezaji yaani kujenga,” anasema.

Kwa mujibu wa Annastazia kazi hiyo haimpi ugumu kwa kuwa moja ya kigezo chake ni kuzingatia kila hatua ya ujenzi , vipimo sahihi na kuwa hilo ndilo limempatia sifa za kazi yake hiyo.

Anakumbuka katika hili isa kimoja, “ kwenye usimamizi wangu wa ujenzi wa majengo niliwahi kumbomolea fundi mmoja tena mtu wa makamu ambaye alijenga tofauti na ramani inavyoelekeza ,alikwenda kinyume na maelekezo yangu.

“Baada ya kumbomolea fundi huyo ukuta mkubwa kutokana na kujenga kinyume na maelekezo yangu, aliamua kuchukua vifaa vyake na kuondoka na hakurudi tena.”

Kitendo hicho kilileta mshangao kwa mafundi wenzake na walieleza kuwa mwenzao alishindwa kutekeleza maelekezo ya msimamizi wa ujenzi kwa kumuona ni binti mdogo.

Annastazia anasema hivi sasa ana kazi anazosimamia ambazo ni ujenzi wa jengo la ghorofa mbili la Shule ya Sekondari Boma, kata ya Boma na mradi mwingine ni ujenzi wa majengo ya Kituo cha AfyaTungi katika Manispaa ya Morogoro.

“Ujenzi wa jengo la ghorafa mbili katika Shule ya Sekondari Boma unaendela na kwa majengo ya Kituo cha Afya Tungi yapo hatua nzuri ya upauaji na ujenzi wake unatarajia kukamilika mwishoni wa mwaka huu,” anabainisha Annastazia.

Binti huyu anajivunia fani yake hiyo kwa kile anacjoeleza kuwa imemfikisha mbali kiujuzi kutokana na kusimamia vyema majengo yote yaliyojengwa yakiwa kwenye viwango bora. Annastazia anasema licha ya kupata changamoto ya kukosa kazi hasa kipindi kigumu cha Corona ,lakini sasa kazi za ujenzi wa majengio ni nyingi na zinapatikana.

“Sasa kazi za serikali zipo nyingi na hata za watu binafsi kinaachohitajika ni kujituma , kujiamini na kusimamia vyema,” anasema Annastazia.

Mbali na kazi yake ya kusimamia ujenzi wa majengo, anasema mkoa wa Morogoro umeanzisha Chama cha Mafundi Ujenzi kinachowashirikisha mafundi wa fani mbalimbali ambacho sasa ni mkombozi kwao.

Anasema amejiunga nacho na wenzake wamemchagua kuwa Katibu wao na kupitia chama hicho wameanzisha mradi wa mashine ya kufyatua tofali kwa lengo la kibiashara ili kuwawezesha wanachama ambao ni vijana kujipatia kipato.

“Serikali ya wilaya ya Morogoro imetupa eneo mtaa wa Boma A , Kata ya Mazimbu na mradi huu ni moja ya nguzo ya kujiajiri sisi wenyewe tujikwamue kiuchumi,” anabainisha.

Annastazia anaeleza kuwa matarajio yake ni kuendelea na masomo ya Chuo Kikuu na kujiendeleza katika taaluma yake hiyo ili kufikia ngazi ya Shahada ya Uhandisi Majengo itakayomuwezesha kuwa nguli wa usimamizi kandarasi kubwa.

“ Nina malengo ya kujindeleza zaidi kielimu katika fani hii ya uhandisi kwani sasa ninapata kazi hizi kwa kuangalia ubora wa kazi ambazo tayari nimezisimamia huko nyuma ambazo zimekidhi viwango vya ubora,” anasema.

Annastazia anaeleza pia ndoto yake ni kumiliki kampuni ya ujenzi itakayomuwezesha kujiajiri na kujingiza kipato na kutoa ajira kwa vijana wengine.

Kwa masuala ya kijamii anasema anapenda kuimba nyimbo za dini na alishawahi kuwa mwimbaji kwenye kwaya ya Vijana Dembezi ya Kanisa la Adventist la mjini Shinyanga na pia aliwahi kupewa uongozi katika kanisa hilo.

“Kweli nina karama za uongozi wa Bwana na uimbaji wa nyimbo za injili na hili nina mshukuru Mungu kunijalia katika kazi zangu hizi, “anasema. Annastazia ni mtoto wa nne kati ya watoto saba wa familia ya Jonathan Charles , kati yao wa kike ni wanne na wa kiume ni watatu.

Elimu yake ya msingi aliipatia katika Shule ya Msingi Mwandui , mkoani Shinyanga na elimu ya kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Sekondari Good Will inayomilikiwa na kanisa la Adventist mjini Shinyanga.

Baada ya kumaliza elimu ya sekondari alijiunga kusomea fani ya usimamizi majengo na barabara katika Chuo cha Ufundi Mbeya (MTC) kwa wakati huo lakini sasa kikitambulika kama Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia( MUST).

Huyo ndio Annastazia, binti anayejiamini na mwenye uthubutu na ndoto ya kuwa mbobezi katika uhandisi majengo.

Related Articles

Back to top button