Mabondia wanawake kwenda Serbia

DAR ES SALAAM: MABONDIA watakaofanya vizuri katika mashindano mapya ya ngumi ya Wanawake ya Samia ‘Samia Women Boxing Championship 2025″ watashiriki michuano ya Dunia itakayofanyika Serbia Machi mwaka huu.
Kwa mujibu wa Rais wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT) Lukelo Willilo, mashindano ya Samia yatafanyika Ijumaa ya wiki hii hadi Februari 2, kwenye fukwe za Kawe beach Dar es Salaam.
Amesema mashindano hayo yatatumika kuchagua wachezaji watakao jiunga na kikosi cha Timu ya Taifa kujiandaa kushiriki kwa mara ya pili katika mashindano ya 14 ya Ubingwa wa Dunia yatakayofanyika Nis, Serbia.
“Hii itakua ni mara ya pili kwa Taifa kushiriki mashindano ya Ubingwa wa Dunia, baada ya kufanya hivyo kwa mara ya kwanza kwanye mashindano ya 13 yaliyofanyika New Delhi, India mwezi wa tatu, 2023
Amesema maandalizi ya mashindano hayo ya Samia yanaendelea vizuri, na kuwaomba wadau wajitokeze kwa wingi kuwaunga mkono kwa hali na mali.
Asha Voniatis, Mwenyekiti wa kamati ya wanawake na wachezaji ya BFT na mjumbe wa kamati ya usawa kijinsia ya Afrika (AFBC) amesema mshindano hayo yatashirikisha wachezaji wanawake wanaocheza ngumi za ridhaa na za kulipwa kupitia kamisheni ya ngumi za kulipwa (TPBRC).
Amesema wachezaji wote watahudhuria pia, semina za kuwawezesha, kuwajengea maarifa ya maisha na ujasiriamali kwa kushirikina na taasisi ya ARHN ya Mbezi Beach, Dar es salaam.
“Wachezaji wote wanawake nchini Tanzania mnaombwa mjitokeze kwa wingi kushiriki mafunzo na mashindano haya,”amesema.