Masumbwi

Ndumbaro atoa agizo kali kwa TPBRC

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt.Damas Ndumbaro ametoa siku saba kwa viongozi wa Kamisheni ya ngumi za kulipwa (TPBRC) kuwasilisha nakala 170  za mikataba zimfikie ofisini kwake.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salam Ndumbaro amesema endapo kama hawatafuata maagizo hayo watafikishwa kwenye vyombo vya dola kwani wameliibia Taifa, wadau wa ngumi, TRA  pamoja na mabondia.

“Natoa agizo Kwa Baraza la Michezo la Taifa BMT kupitia kwa Katibu Mtendaji wake Neema Msitha nataka nakala hizo zinifikie, zisipofika wale wote waliohusika tutawafikisha kwenye vyombo vya dola, alisema Ndumbaro.

Amesema suala hilo hawatalifumbia macho kwani linachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha  nyuma mchezo wa ngumi na kusababisha vijana wengi kukosa ajira.

 

Waziri Ndumbaro amesema miongoni mwa hoja 13 ambazo zimetolewa na Kamati ya Uchunguzi ni ile ya matumizi ya shilingi  milioni 183.3ambazo hazina udhibitisho, ni fedha nyingi ambazo ni jasho la mabondia na kudai amesikitishwa  na kitendo hicho kwa kiasi kikubwa.

“Ukikosa uthibitisho kwenye matumizi  ni wizi, lazima ulete nyaraka za uthibitisho zinazoonyesha jinsi fedha hizo zilivyotumika kwani hizo ni fedha nyingi ambazo mabondia wametumia jasho lao,” amesema Waziri Ndumbaro.

Amepongeza  Kamati hiyo ya uchunguzi kutokana  na kufanya kazi yao kwa weledi na kubaini hoja  ambazo zina mashiko makubwa.

 

Katika hatua nyingine alimtaka  msajili wa vyama vya michezo nchini Evodi Kyando  aipitie ripoti hiyo ili aweze kuchukua hatua stahiki dhidi ya viongozi hao.

“Msajili uchukue hatua kali zile za jinai zipelekwe kwenye vyombo vya jinai na wataendelea kuusimamisha mpaka hapo msajili atakaposema wana hatia au la!,bila upendeleo wala kuonea mtu yeyote, amesema.

Hata hivyo ameongezea siku 90 nyingine Kamati hiyo kutokana na kuridhishwa na kazi iliyofanya pamoja na kuwaongeza viongozi wengine ambao wataungana na Kamati hiyo.

Related Articles

Back to top button