Kaoneka atamba kushusha kipigo

BONDIA Shaban Kaoneka amesema baada ya kimya cha muda mrefu anarejea ulingoni usiku wa mabingwa ambapo awamu hii amepanga kushusha kipigo kwa Shaban Ndaro.
Kaoneka anatarajiwa kupanda ulingoni Desemba 26, mwaka huu katika pambano la kumsindikiza bondia Mfaume Mfaume atakayechuana na Idd Pialal mkoani Arusha.
Akizungumza na gazeti la HabariLEO Dar es Salaam, Kaoneka amesema kwa mazoezi anayofanya anataka kurudi ulingoni kwa kasi na kuahidi kumfundisha nidhamu mpinzani wake.
“Wananchi wa Mbagala wamenituma nimfundishe adabu Ndaro, naendelea na maandalizi
mazuri kuhakikisha nampa kipigo mpinzani wangu ambacho kitamfunza adabu,” amesema.
Amesema anajua mpinzani wake sio mbaya ila hatamuacha salama, ni lazima apate kipigo
kikali siku hiyo.
Kaoneka atakumbukwa namna alivyompiga bondia Karim Mandonga katika pambano
ambalo licha ya kushinda kwa ‘Technical Knockout’ katika raundi ya nne, alipata umaarufu
mpinzani wake lililochezwa Songea mkoani Ruvuma.
Tangu Kaoneka acheze pambano hilo na kushinda hajaonekana tena ulingoni na huenda
akarudi kivingine.
Wengine watakaopanda ulingoni siku hiyo ni Hamadi Furahisha dhidi ya Grey Chimkwapulo, Yohana Mchanja dhidi ya Haidary Mchanjo, Batuli Yassin dhidi ya Loveness Kokha, Osama Arabi dhidi ya Said Faraji na Ramadhan Rajabu dhidi ya Rashid Ngosha.