Kamwe: Pacome bado ni wetu

DAR ES SALAAM: MENEJA wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, amesema kiungo Pacome Zouzoua bado ni mchezaji wa klabu hiyo na anaendelea kupata stahiki zake zote, huku akieleza kuwa anaendelea vizuri katika mchakato wa kupona baada ya kufanyiwa upasuaji.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu Pacome, Kamwe amesema maendeleo ya Pacome ni makubwa baada ya kufikisha takribani miezi mitatu tangu alipofanyiwa upasuaji, akibainisha kuwa kwa sasa mchezaji huyo anaweza kukanyaga mguu, tofauti na awali alipokuwa hawezi kufanya hivyo.
“Pacome anaendelea vizuri haimaanishi kwamba anaweza kukimbia. Ni maendeleo baada ya kufanyiwa upasuaji. Kwa sasa mguu unakanyaga, anaweza kukanyagia maumivu, wakati awali alikuwa hawezi kukanyaga. Kwa hiyo ni maendeleo makubwa,” amesema Kamwe.
Amesema mashabiki wanapaswa kuelewa kuwa maendeleo hayo hayamaanishi Pacome yuko tayari kurejea kucheza, bali bado anaendelea na hatua za matibabu na urejeshaji wa uwezo wake wa mwili.
Kamwe amesema licha ya Pacome kutolewa kwa muda kwenye mfumo wa timu kutokana na majeraha, bado ana mkataba na Yanga na klabu inaendelea kumtambua kama sehemu ya timu.
Ameongeza kuwa hata pale timu inapopata mgao wa bonasi baada ya kushinda mchezo, Pacome bado anahusishwa kwa mujibu wa utaratibu wa klabu, akisisitiza kuwa Yanga inaendelea kumchukulia kama sehemu kamili ya familia yake.
Kamwe amesema Pacome anatarajiwa kufika Azam Complex Jumamosi kuwaona wachezaji wenzake ambao amekuwa mbali nao kwa muda, huku pia akipata nafasi ya kukutana na mashabiki wa Yanga katika mchezo wa marudiano dhidi ya Gaborone United.
Amesema klabu inaendelea kumpa muda na mazingira mazuri ya kupona kikamilifu, huku ikisubiri wataalamu wa afya kuamua wakati sahihi wa kurejea kwake katika ushindani.




