Simba yaua, Ahoua wa moto

DAR ES SALAAM: Kiungo mshambuliaji wa Simba, Jean Charles Ahoua, ameendelea kuthibitisha kuwa yeye ni hatari mbele ya lango baada ya kuonesha uwezo wa hali ya juu kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Nyota huyo kutoka Ivory Coast ameweka rekodi ya mabao 12, akiwapiku washambuliaji wa Yanga, Clement Mzize na Prince Dube, ambao wamefunga mabao 10 kila mmoja.
Katika mchezo wa kiporo dhidi ya Dodoma Jiji FC, uliopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Ahoua alifunga mabao mawili, akisaidia Simba kuibuka na ushindi mnono wa 6-0. Ushindi huu umewaweka Wekundu wa Msimbazi katika nafasi nzuri kwenye mbio za ubingwa.
Simba ilianza mchezo kwa kasi, ambapo Elie Mpanzu alifungua karamu ya mabao dakika ya 16. Baada ya hapo, Ahoua alitikisa nyavu mara mbili dakika ya 21 na 45, akionesha uhodari wake wa kufumania nyavu.
Kipindi cha pili kilianza kwa moto zaidi, huku Steven Mukwala akiongeza bao la nne dakika ya 46, baada ya kazi nzuri ya Mpanzu, hatimaye, Denis Kibu alihitimisha ushindi huo kwa bao la tano na sita dakika ya 54 na 70.
Kwa ushindi huu, Simba inaendelea kuonesha ubabe wake, huku Ahoua akizidi kuimarika kama kinara wa mabao msimu huu. Mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi wanazidi kupata matumaini makubwa ya kutwaa ubingwa wakiwa na alama 57 nafasi ya pili akizidiwa alama moja na Yanga kwa alama 58.