Nyavu

Wavu moto kuelekea mtoano

DAR ES SALAAM: VITA ya ubingwa, nafasi za kufuzu msimu ujao na kuepuka kushuka daraja imeifanya Ligi ya Taifa ya Mpira wa Wavu kuwa na ushindani mkubwa kuelekea hatua ya mtoano itakayoanza Septemba 14 hadi 19 mwaka huu.

Mzunguko wa pili wa ligi hiyo ulioanza Septemba 6 unatarajiwa kumalizika Septemba 13, kabla ya timu zinazofuzu kuingia kwenye hatua ya robo fainali, nusu fainali na hatimaye fainali zitakazotoa bingwa wa msimu wa 2026.

Mkurugenzi wa Utawala wa Shirikisho la Wavu Tanzania na Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi ya Mpira wa Wavu Tanzania, Riziki Godwin, amesema ushindani umeongezeka kutokana na kila timu kupambana kutimiza malengo yake katika hatua hiyo muhimu ya msimu.

“Tunapofikia mzunguko wa pili maana yake ni mzunguko wa mwisho ambao unatoa bingwa, lakini pia unatoa timu zinazofuzu kucheza ligi ya msimu ujao na zile zinazoshuka daraja,” amesema Godwin.

Amesema hali hiyo imefanya kila mchezo kuwa na umuhimu, kwani baadhi ya timu zinapambana kwa ajili ya ubingwa wakati nyingine zikitafuta nafasi ya kubaki kwenye ligi.

Kwa upande wa wanawake, Godwin amesema timu kama Bandari, JKT Stars na Korosho zimeonesha ushindani mkubwa na ziko katika nafasi nzuri ya kuwania hatua ya mwisho, huku Chui na Kampala nazo zikiendelea kutoa upinzani.

Kwa wanaume, amesema Bandari, JKT Stars, Milambo, JKT na Tanzania Prisons ni miongoni mwa timu zinazofanya vizuri na kuonesha ushindani mkubwa katika mbio hizo

Related Articles

Back to top button