Barker: Hatutaki kufanya kosa

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Simba, Steven Barker, amesema kikosi chake kimejifunza kutokana na mchezo wa kwanza dhidi ya Mighty Wanderers na sasa kinaingia kwenye mchezo wa marudiano kikiwa tayari kupambana hadi kuhakikisha kinapata ushindi.
Barker amesema wamefanya uchambuzi wa mchezo uliopita ili kubaini maeneo ambayo hawakufanya vizuri na kuyafanyia kazi kabla ya mchezo huo.
“Tumejifunza mambo mengi kutokana na mchezo uliopita. Jambo muhimu kwa sasa ni kuhakikisha tunafanyia kazi maeneo ambayo tuliona hatukuwa katika kiwango tulichotaka,” amesema.
Amesema kucheza nyumbani kunawapa Simba nafasi ya kutumia nguvu na msukumo wa mashabiki kuhakikisha wanapata ushindi na kusonga mbele katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Tunapocheza nyumbani tunataka kushinda kila mchezo wa Ligi ya Mabingwa. Hilo ndilo litakalokuwa lengo na mpango wetu kuhakikisha tunapata ushindi mbele ya mashabiki wetu,” amesema.
Barker amesema hawataki kufanya kosa la kufikiri kwamba tayari kazi imekwisha kutokana na matokeo ya mchezo wa kwanza, akisisitiza kuwa bado wana kazi ya kufanya.
“Itakuwa ni kosa kubwa sana kwetu kufikiri kwamba tayari tumemaliza mechi. Tunajua bado haijaisha, ndiyo maana tunajiandaa kwa umakini mkubwa kulingana na hali hiyo,” amesema.




