Ligi Kuu

Zimbwe Jr: Hatuna presha, tumejiandaa

DAR ES SALAAM: BEKI wa Yanga, Mohamed Hussein ‘Zinbwe Jr’, amesema kikosi hicho hakina presha kuelekea mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United, akisisitiza kuwa maandalizi wanayofanya yanawapa matumaini ya kupata matokeo mazuri na kusonga mbele.

Yanga ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Gaborone United katika mchezo wa kwanza uliochezwa Botswana, hivyo sasa inaingia kwenye mchezo wa marudiano ikiwa na nafasi ya kutumia faida ya uwanja wa nyumbani kutafuta ushindi na tiketi ya hatua inayofuata.

Tshabalala amesema wachezaji wamekuwa wakifanya maandalizi mazuri chini ya benchi la ufundi na hawana sababu ya kuingia kwenye presha, kwani wanachotakiwa ni kutekeleza maelekezo ya makocha kwa umakini.

“Hatuna presha kabisa. Mpira ni mchezo wa maandalizi na maandalizi tunayofanya yanaashiria kwamba tunafanya vizuri kuelekea mchezo,” amesema Zimbwe Jr.

Amesema mchezo wa kwanza umewapa nafasi ya kuona ubora na mapungufu ya wapinzani wao, huku akibainisha kuwa moja ya maeneo waliyoyatambua ni mipira ya kufa ambayo Gaborone United imekuwa ikitumia.

Ameongeza kuwa makocha wanaendelea kuwapa maelekezo kuhusu namna ya kukabiliana na maeneo hayo, huku wachezaji wakilenga kupunguza makosa yaliyotokea katika mchezo wa kwanza na kufanya vizuri zaidi kwenye marudiano.

Zimbwe Jr amesema baada ya kupata sare ugenini, sasa jukumu lao ni kuhakikisha wanatumia mchezo wa nyumbani kupata matokeo yatakayowapa nafasi ya kusonga mbele, huku akisisitiza kuwa lengo ni kuwapa furaha mashabiki na Watanzania kwa ujumla.

Amesema pia wamepokea kwa furaha mpango wa Yanga kumuenzi Selemani Mwalimu siku ya mchezo huo, akiamini tukio hilo litaongeza hamasa kwa wachezaji kufanya vizuri uwanjani.

“Sisi kama wachezaji tunapaswa kufanya kazi yetu uwanjani. Bila sisi kufanya vizuri, kucheza kwa kiwango kizuri na kupata matokeo, heshima hiyo haitakuwa na maana kubwa,” amesema.

Related Articles

Back to top button