Ligi Kuu

JKT Tanzania yatamba licha ya sare

DAR ES SALAAM: JKT Tanzania imeonesha kiwango cha kujiamini kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Les Aigles du Congo katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Samweli.

Akizungumzia mchezo huo, Ofisa Habari na Mawasiliano wa JKT Tanzania, Masau Bwire, amesema kikosi hicho kilionesha kiwango kizuri licha ya wapinzani wao kurejea kwenye mchezo na kusawazisha.

Bwire amesema mchezo huo ulikuwa kipimo muhimu kwa JKT Tanzania, hasa baada ya Aigles du Congo kuonesha ubora wao katika mchezo wao dhidi ya Yanga, ambapo waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika tamasha la Yanga Day.

Amesema Aigles du Congo walivutiwa na kiwango cha JKT Tanzania na aina ya soka linalochezwa na timu hiyo, jambo lililowafanya kuwasiliana na uongozi wa klabu kwa ajili ya kupata mchezo huo wa kirafiki.

Kwa mujibu wa Bwire, licha ya matokeo kuwa sare, JKT Tanzania ilipata faida kubwa kutokana na mchezo huo kwa kupata uzoefu na kujipima dhidi ya timu yenye ushindani wa kimataifa.

Mchezo huo pia ni sehemu ya maandalizi ya JKT Tanzania kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu, ambapo itaanza kampeni yake Agosti 16 kwa kuikaribisha TRA kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.

Bwire amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kuisapoti JKT Tanzania, akisisitiza kuwa kikosi hicho kiko tayari kwa ushindani wa msimu mpya.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button