Arteta: Hatujapoteana
LONDON: Kocha wa Arsenal Mikel Arteta amesema kikosi chake bado hakijaondoka kwenye mbio za ubingwa wa Ligi kuu ya England licha ya matokeo mabaya ya hivi karibuni.
Arteta ambaye kikosi chake kimekuwa kikitoa upinzani mkali kwa mabingwa Manchester City kwa misimu miwili iliyopita aliulizwa juu ya tofauti ya alama zilizopo kati yao na vinara wa ligi kwa sasa Manchester City na Liverpool ambao wanaonekana kutaka kitu msimu huu
“Kama unataka kuwa wa kwanza inabidi kushinda kila mchezo kuwa wa kwanza. Tunajua namna ambavyo tunapaswa kucheza kukabiliana na ushindani msimu huu, Hatujapoteana.” amesema
“Tunajua mchezo wa kesho ni mgumu kiasi gani, tumejiandaa na tutakabiliana na kila lijalo kesho, tuko tayari kabisa.” ameongeza
Gunners walio nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi wako nyuma ya vinara Manchester City baada ya kuduwazwa kwa mabao 2-0 na Bournemouth kisha sare ya 2-2 na Liverpool, wakitarajia kusafiri kukipiga na Newcastle United kesho Jumamosi.
Arteta amesema pia bado atawakosa beki Riccardo Calafiori na Martin Odegaard katika mchezo huo utakaochezwa St James’ Park huku Takehiro Tomiyasu akiwa bado hayupo. Arteta pia hana uhakika kuhusu kupatikana kwa Ben White lakini Gabriel Magalhaes anaweza kuwa dimbani.
Newcastle United wako nafasi ya 12 kwenye kwenye msimamo wa Ligi, bila ushindi wowote katika mechi zao tano zilizopita, lakini Arteta ametahadharisha kuwa bado wanaweza kuwa tishio.